'Ulaji hafifu shuleni unaathiri maendeleo ya akili'
Muktasari:
- Wadau wa lishe wameshiriki mjadala wa Mwananchi X Space wenye mada ‘Umuhimu wa kuwapa chakula mchanganyiko watoto wa shule’ na kutoa ushauri mbalimbali kwa wananchi kuzingatia lishe bora.
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kimesema ulaji hafifu shuleni utachangia watoto kukosa akili ya maisha na kujikwamua kutoka katika umaskini pale watakapokuwa wakubwa.
Wakati SUA ikieleza hayo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), limesema ili wanafunzi wafikie malengo yao, wafaulu, wakue na wawe makini darasani wanapaswa wapate lishe nzuri.
Wadau hao wamesema hayo leo Jumatatu Agosti 12, 2024 wakati akichangia mjadala kwenye Mwananchi X Space, inayoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania pamoja na Taasisi ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC) wenye mada isemayo ‘Umuhimu wa kuwapa chakula mchanganyiko watoto wa shule.’
Profesa wa Lishe kutoka SUA, Joyce Kinabo akizungumza katika mjadala huo amesema ulaji hafifu shuleni utachangia watoto kukosa akili ya maisha na kujikwamua kutoka katika umaskini pale watakapokuwa wakubwa.
Amesema lishe bora ina umuhimu mkubwa kwa watoto ambao wanatakiwa kuja kuhimili maisha wanayoyaendea, hivyo wanapaswa kulishwa vyakula mchanganyiko. Amesema watoto wanapata mabadiliko ya kimwili, hivyo wanapaswa kupata virutubisho mbalimbali.
“Kama Taifa likishindwa kulisha ubongo wa watoto, basi tujihesabu tumeshindwa. Tuhakikishe watoto wetu wanapata vyakula vitakavyowakuza vizuri na wawe na akili za kutosha.
“Mabadiliko ya kimwili ndio yanayoendeleza mahitaji ya lishe na inapatikana katika vyakula mbalimbali, kwa wastani mwili wa binadamu unahitaji virutubisho zaidi ya 40 kwa siku vinavyopatikana katika vyakula mbalimbali,” amesema.
Profesa huyo amesema ndio maana kuna mbogamboga, matunda, nyama, dagaa, marahage na jamii ya mikunde na vinashirikiana katika matumizi yake mwilini.
Aidha, ameshauri vyakula vinavyouzwa nje ya nchi vinatakiwa kuwalisha watoto wetu, ili wapate akili na ufanisi.
“Uwezo wa kuwalisha vyakula tunao, tunachotakiwa ni kujipanga kama Taifa na njia zipo nyingi kuanzia kuhamishisha wazazi wajue faida za kuwalisha watoto vyakula mchanganyoko, basi kila mtu atakuwa tayari kuchukua nafasi yake ili kuchangia ubora wa vyakula shuleni pamoja na mazingira,” ameshauri Profesa Kinabo.
Kwa upande wake, Ofisa Lishe Taifa kutoka WFP, Deborah Esau amesema ili wanafunzi wafikie malengo yao, wafaulu, wakue na wawe makini darasani wanapaswa wapate lishe nzuri.
Amesema endapo wakila makande, uji au chai kavu wanakosa virutubisho, kwani kwa ujumla mwili wa binadamu ili ufanye kazi kwa ufanisi unahitaji lishe bora.
“Mwanafunzi anapitia mabadiliko mengi kama kimwili, kitabia na hivyo lishe bora ni muhimu katika kipindi hicho,” amesema ofisa huyo.
Amesema kutokana na hali ya kiuchumi ya familia nyingi, ndio maana Shirika la WFP linasaidia kuiwezesha Serikali kujitegemea ili kutoa huduma ya chakula shuleni.
“Kwa sasa tunasadia shule zilime ili zipate chakula, mfano huko Kigoma, tunasaidia mbegu na utaalamu kuhakikisha miradi hiyo ifanikiwe, pia tunazishauri halmashauri zitenge bajeti shuleni, mfano shule zenye mashamba ili watoto wapate chakula” amesema.
Akizungumza katika mjadala huo, Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC), Maria Ngilisho, amesema chakula mchanganyiko kwa watoto kinaanzia na kifungua kinywa cha asubuhi wanapoondoka kwenda shuleni.
Amesema mlo huo ni muhimu na unampatia nguvu katika siku yake anapokwenda kwenye masomo, kwani inawafanya wafuatilie masomo yao kwa ufanisi.
“Baadhi ya tafiti zimetuonyesha mtoto akipata kifungua kinywa anahudhuria masomo na inamuweka mazingira salama na kumuepusha na vishawishi hatarishi kama kurubuniwa,” amesema.
Amesema tafiti zilizofanyika Mkoa wa Dar es Salaam, zimebaini watoto wengi wanatoka kwenda shule bila kupata kifungua kinywa na wale wanaopata shuleni hawapati viliyo bora, wanapata vyenye rangirangi na mafuta mengi
Hivyo, amehimiza watoto wapate vifungua kinywa kabla hawajaenda shuleni, washibe wapate nguvu na virutubisho waepukane na kurubuniwa na matatizo mengine.