Umri wa urais na gumzo kwa Watanzania

Wednesday November 25 2020
umri pic
By Peter Elias

Upi ni umri sahihi wa mtu kuwa Rais wa nchi? Pengine Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa jibu juu ya swali hilo. Lakini mtu wa umri gani hana sifa ya kuwa Rais? Huo ni mjadala.

Hoja hiyo imeendelea kujadiliwa na makundi mbalimbali ya rika tofauti ya Watanzania baada ya Rais John Magufuli kuweka bayana kwamba hataruhusu Rais ajaye amzidi umri.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo Novemba 16 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati wa hafla ya kumwapisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na mawaziri wawili ambao aliwateua wiki mbili zilizopita.

Mawaziri pekee walioapishwa na Rais Magufuli ni wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kupendekeza kwenye Kamati Kuu yake jina la mtu mwenye umri mkubwa, badala yake wanatoa nafasi kwa vijana ambao wanakubalika zaidi kwa sasa na Watanzania wengi. Rais Magufuli alitoa mifano ya viongozi mbalimbali ambao hawakuutafuta uongozi huku akiwatahadharisha baadhi ya viongozi kutotumia fedha zao kuutafuta urais kwa sababu hawawezi kuupata kwa sababu ya umri mkubwa walionao.

“Hakuna mtu alitegemea (Hussein) Mwinyi atakuwa Rais wa Zanzibar, lakini pia Mwinyi katika kipindi chake chote hakuutafuta urais. Vitu hivi vinapangwa…” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

Advertisement

“Hakuna mtu alijua Profesa Ibrahim (Juma) atakuwa Jaji Mkuu, hata mimi sikujua kama nitakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu katika miaka yangu yote 20 nikiwa waziri na nikiwa mbunge, sikuwahi kuomba hata ujumbe wa NEC.

“Wajumbe wa NEC walikuwa akina Lukuvi, tangu aingie mle ni mjumbe wa NEC, lakini urais hakuupata na sina uhakika kama ataupa urais. Sasa hivi ana miaka sitini na kitu, tukapendekeze kwenye central committee tuchague Rais anayenizidi umri mimi?” alihoji mkuu huyo wa nchi.

Mbali na kumtaja Lukuvi kama mmoja wa watu ambao hawawezi kuwa marais katika Taifa hili, Rais Magufuli alimtaja pia Waziri Kabudi pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela ambao wote wamemzidi umri.

Hata hivyo, Ibara ya 39 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema; “Mtu hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kama ametimiza umri wa miaka 40. Kauli hiyo ya Rais Magufuli imepokelewa kwa hisia tofauti na wadau mbalimbali wa siasa, baadhi yao wakisema sifa za mtu husika ndiyo ziangaliwe badala ya umri wake na wengine wakieleza kuwa anaamini katika uwezo wa vijana.

Mchambuzi wa siasa na kada wa chama cha UDP, Andrew Bomani aliliambia Mwananchi kuwa hoja ya kuwa na Rais kijana ilianza wakati wa Jakaya Kikwete alipogombea urais mwaka 2005, akiitumia kama mtaji wake wa kisiasa.

Hata hivyo, Bomani alisema kitu muhimu cha kuangalia sifa za mtu anayetaka kuwa Rais na umri wake usiwe kizuizi cha kumfikisha katika malengo yake ya kuwatumikia Watanzania.

“Ni wakati wa kuangalia sifa za mtu na wakati mwingine sifa zinakwenda pamoja na uzoefu wa mtu. Suala la umri lisiwe kikwazo, tuangalie sifa alizonazo mtu anayeomba urais,” anasema Bomani.

Anatoa mfano wa Rais mteule wa Marekani, Joe Biden ambaye ameteuliwa kuwa Rais wa Taifa hilo akiwa na umri wa miaka 78 na kuweka rekodi ya kuwa Rais aliyechaguliwa akiwa na umri mkubwa zaidi. Alisisitiza kwamba Wamarekani hawajaangalia umri wake bali sifa alizonazo.

Akiwa na mtazamo kama huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala anasema Rais Magufuli alitoa mawazo yake na huenda angependa vijana ndiyo waongoze Taifa hili. Hata hivyo, alipingana naye akisema yoyote mwenye sifa anafaa kuwa Rais bila kujali umri wake. Anasema wapo viongozi walioanza uongozi wakiwa vijana na wakafanya vizuri, mfano Mwalimu Julius Nyerere, lakini pia alisema wapo waliopata uongozi wakiwa wazee na wakafanya vizuri.

“Ni kawaida kwa Rais anayeondoka madarakani kuandaa mtu atakayemrithi, bila shaka ana mtu ambaye anaona anafaa kurithi nafasi yake,” alisema Profesa Mpangala.

Katibu Mkuu wa Chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo alisema kauli ya Rais Magufuli imeweka msingi wa matumaini kwa vijana lakini pia amewakumbusha wanaomzunguka wasiutarajie urais katika umri wao mkubwa.

Doyo anasema Magufuli anawajenga vijana kushika nafasi hiyo ya juu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiaminika kwamba wenye umri mkubwa ndiyo wenye uwezo wa kuitumikia.

Mwanasiasa huyo ametoa rai kwa mamlaka husika kufikiria kupunguza umri wa wagombea urais kutoka miaka 40 inayopendekezwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili vijana wengi zaidi wajitokeze kuwania nafasi hiyo nyeti.

Hata hivyo, mwanasheria mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotaja jina lake, alisema kauli ya Rais Magufuli haina nguvu kisheria kwa sababu Katiba ya nchi haijaweka ukomo wa umri kwa mtu anayetaka kugombea urais.

Advertisement