Utata gawio la mashirika

Utata gawio la mashirika

Muktasari:

  • Madeni makubwa na mtaji mdogo wa mashirika ya umma yaliyobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huku taasisi hizo zikitoa gawio serikalini, yameibua mjadala wa wadau wanaoshangazwa na hali hiyo.

Dar/Dodoma. Madeni makubwa na mtaji mdogo wa mashirika ya umma yaliyobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huku taasisi hizo zikitoa gawio serikalini, yameibua mjadala wa wadau wanaoshangazwa na hali hiyo.

Mjadala huo umeibuka baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuziita bodi na menejimenti za mashirika hayo kujadili ripoti ya CAG ya mwaka 2019/20 inayobainisha udhaifu katika maeneo kadhaa unaopunguza ufanisi.

Mjadala huo umeibuka zikiwa zimepita siku chache tangu PAC ilipoeleza kushangazwa na deni la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lisiloendana na mtaji wake huku Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) likiwa na madeni yanayohitaji kusimamiwa haraka iwezekanavyo.

Katika uchambuzi wake, PAC imesema CAG amebaini TTCL ina madeni ya Sh403 bilioni wakati mtaji wake ni Sh243 bilioni, hivyo kupungukiwa mtaji kwa Sh132 bilioni, jambo linaloashiria kuwa na ufanisi usioridhisha.

Wakati hali ikiwa hivyo, baadhi ya wananchi wamekumbusha ilivyokuwa mwaka juzi shirika hilo lilipojitokeza kutoa gawio la Sh2.1 bilioni lililoongezeka kwa Sh600 milioni zaidi ya kiasi kilichotolewa mwaka 2018 kutokana na kuimarika kwa faida yake.

Akikabidhi gawio hilo (Mei 21, 2019), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL, marehemu Omar Nundu alisema gawio hilo ni kwa mwaka wa fedha wa 2017/18.

Kutokana na hoja hizo zinazojadiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amelazimika kufafanua akisema deni halizuii shirika au taasisi kupata faida wala kumzuia mwenye mali (Serikali) kuongeza mtaji.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Kindamba aliandika: “Kwa kuwa kutoa gawio ni takwa la kisheria, faida au hasara ni matokeo ya mauzo yako ukitoa gharama zako za uendeshaji ndani ya mwaka husika wa kibiashara na hapo ndipo linapozaliwa gawio au kinyume chake na kwa kuwa kulikuwa na faida sheria inataka utoe gawio.”

Kwenye ripoti yake, CAG amebainisha kampuni tanzu za mashirika ya umma yaliyopata hasara mfululizo kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na kuwa na kiasi kidogo cha wateja na kutofanya kazi kikamilifu ikiwamo TTCL Pesa, inayomilikiwa kwa ubia kati ya TTCL yenye asilimia 99 na Ofisi ya Msajili wa Hazina asilimia moja.

Wabia hao kwa pamoja wamewekeza Sh2.48 bilioni lakini kampuni ilipata hasara ya Sh410 milioni mwaka 2019/20 iliyopungua kutoka Sh690 milioni ya kwama 2018/19.

CAG pia amesema TTCL ni miongoni mwa taasisi 23 zenye upungufu wa watumishi 4,092 sawa na asilimia 37 ya kiwango kilichopendekezwa cha watumishi 11,122. TTCL inatakiwa kuwa na watumishi 1,424 ina upungufu wa 117.

Akizungumzia utata unaojadiliwa mtandaoni, Msajili wa Hazina, Benedictor Mgonya alisema ofisi yake ni kama mlezi wa mashirika ambayo kila moja lina mzazi wake ambaye ni wizara husika.

“Yapo yanayojiendesha kibiashara kama TTCL au Benki ya NMB ambako Serikali ina hisa, hawa hutoa gawio kulingana na faida iliyopatikana halafu kuna yanayotoa huduma, yenyewe hutoa CSR (fungu la kusaidia jamii),” alisema Mgonya.

Kuhusu madeni ya TTCL, Mgonya alisema ni ya kihistoria na “mengine hayaeleweki yalivyopatikana.”

Akijadili hali hiyo, Mchumi na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Abel Kinyondo alisema kuna mitazamo miwili ambayo ni upande wa kibiashara na huduma. Kibiashara, alisema shirika inabidi lipate faida ndipo bodi iidhinishe gawio kwa wanahisa na kihuduma alisema kutoa gawio ni lazima.


Madeni makubwa NHC

Kwenye kikao cha PAC jana, Makamu Mwenyekiti wake, Japhet Hasunga alisema shirika hilo linazidai taasisi za Serikali Sh26.75 bilioni, hivyo kulifanya lijiendeshe kwa shida na hivyo akayataka yalipe fedha hizo.

Baadhi ya wadaiwa wa NHC ni Wizara ya Afya (Sh692 milioni), Tume ya Haki za Binadamu (Sh313 milioni), Wizara ya Ardhi (Sh267.6 milioni) na iliyokuwa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo (Sh250.6 milioni).

Alipoulizwa kuhusu madeni ambayo wizara yake inadaiwa na NHC, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alisema “sina taarifa,” hata alipoambiwa ni yale yaliyobainishwa kwenye ripoti ya CAG bado alisisitiza: “Sina taarifa hizo.”

NHC ni miongoni mwa mashirika yenye kampuni zinazopata hasara mfululizo. Shirika hilo linamiliki asilimia 50 kwenye Kampuni ya Uwekezaji ya NHC & PPF NHC huku asilimia 50 zikimilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambako Sh6.40 bilioni zimewekezwa lakini ilipata hasara ya Sh1.38 bilioni mwaka 2019/20 kutoka hasara ya Sh1.07 bilioni mwaka 2018/19.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Profesa Haji Semboja alisema katika mifumo ya kimataifa, gawio hutolewa kwa makubaliano ya kisheria.

“Tulipohitaji fedha kwa ajili ya ujenzi miradi, watu walijitokeza…ni innovation ambayo siikatai. Ni kwa sababu tulikuwa na mahitaji ya haraka ziweze kutekeleza miradi mikubwa kama SGR na bwawa la umeme,” alisema Profesa Semboja.