Vibanda kando ya barabara jijini Dar es Salaam kuondolewa

Vibanda kando ya barabara jijini Dar es Salaam kuondolewa

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri amewataka wafanyabiashara  waliojenga vibanda katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuviondoa kabla ya Mei 18, 2021.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri amewataka wafanyabiashara  waliojenga vibanda katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuviondoa kabla ya Mei 18, 2021.

Wakati Shauri akieleza hayo, gari lenye spika za matangazo linapita katikati la mitaa ya Jiji hilo likitangaza kuhusu  mchakato huo kwamba vibanda havitakiwi kuonekana kando ya barabara.

Akizungumza na Mwananchi Digitial  leo Jumanne Mei 11, 2021 Shauri amesema hawajazuia wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao,  wanachotakiwa kufanya ni kutojenga vibanda na kuwataka wauze bidhaa zao kwenye meza ili wakimaliza iwe rahisi kuziondoa na kuacha maeneo wazi.

Amebainisha kuwa sheria ya mipango miji hairuhusu kujenga vibanda, kuwataka wafanyabiashara hao kutii agizo hilo.

“Mwisho Mei 18 kama ambavyo gari la matangazo linavyotangaza waviondoe vibanda vyao kwa sababu vingine vinajengwa hadi kwenye njia za watembea kwa miguu na barabarani na kuleta adha kwa watumiaji. Wanatakiwa watii sheria bila shuruti waviondoe wenyewe,” amesema Shauri.