Vifo vilivyotokana na moto, majanga 2021 hivi hapa

Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Puyo Nzalayaimisi

Muktasari:

  • Watu 32 walipoteza Maisha na wengine 145 kujeruhiwa katika matukio ya moto 1803 yaliyotokea kati ya Januari hadi Desemba 2021.

Dodoma. Watu 32 walipoteza Maisha na wengine 145 kujeruhiwa katika matukio ya moto 1803 yaliyotokea kati ya Januari hadi Desemba 2021.

Kauli hiyo imetolewa Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Puyo Nzalayaimisi  leo Jumatano Januari 5,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya matukio kwa mwaka ulioishia Desemba 2021.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Nzalayaimisi mbali na matukio hayo ya moto, lakini watu wengine 388 walipoteza maisha kwenye matukio mbalimbali.

Alisema kwa mwaka huo kulikuwa na jumla ya matukio 694 ambayo mbali na vifo yalisababisha majeruhi 763.

Miongoni mwa matukio hayo ni ajali za barabarani, mafuriko, kuzama migodini,mashimo ya vyoo,visima,moto,baharini na maeneo mengine.

"Katika kipindi hicho, karibu matukio 10 yalikuwa ni kwa watoto kutumbukizwa katika mashimo ya vyoo na maeneo yaliyoongoza kuwa na matukio mengi ni mikoa ya nyanda za juu kusini," amesema Nzalayaimisi.

Msemaji huyo ameelezea mkakati wanaofanya kupunguza majanga ni kuendelea kutoa elimu ambapo kwa mwaka uliokwisha walifikia maeneo 2,474 na jumla ya watu 197,183 walinufaika na Elimu hiyo.

Kuhusu changamoto ya uzimaji moto katika majengo marefu amesema kwa sasa wana kikosi maalum chenye mafunzo kwa ajili ya kuzima moto wa juu hivyo hawana shida tena.

Amewataka wananchi kabla ya kujenga wafuate ushauri na sheria inavyowataka kuwa lazima wapitishe ramani zao kwa wataalamu wa Zimamoto ili kuondoa usumbufu majanga yanapotokea.