Viti maalum Chadema pasua kichwa

Muktasari:

Oktoba 31, mwaka huu Chadema na ACT Wazalendo vilitoa tamko la kutoutambua uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 na kutaka urudiwe sambamba na ule wa Zanzibar na usimamiwe na tume huru lakini sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inakamilisha utaratibu wa kuwateua wabunge wa viti maalumu huku chama hicho kikiwa na sifa zinazohitajika kutoa wawakilishi hao.

Moshi. Ama wapeleke au wasipeleke majina ya wabunge wa viti maalum ndio swali linalogonga vichwa vya viongozi wa Chadema, chama kikuu cha upinzani.

Oktoba 31, mwaka huu Chadema na ACT Wazalendo vilitoa tamko la kutoutambua uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 na kutaka urudiwe sambamba na ule wa Zanzibar na usimamiwe na tume huru lakini sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inakamilisha utaratibu wa kuwateua wabunge wa viti maalumu huku chama hicho kikiwa na sifa zinazohitajika kutoa wawakilishi hao.

Msimamo wa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi mkuu ndio unakifanya Chadema kipate kigugumizi kuwaruhusu wabunge wake kuingia bungeni. Iwapo itafanya hivyo, itakuwa sawa na kuuhalalisha uchaguzi kinaosema haukuwa huru wala wa haki.

Ingawa idadi ya wabunge wa viti maalum inaostahili kupata kulingana na wingi wa kura za wabunge wa majimbo haijawekwa wazi, taarifa kutoka ndani ya Chadema inasema ni 22.

Taarifa zaidi zinajuza kuwa uteuzi huo ulikuwa moja ya ajenda za kikao cha kamati kuu kilichofanyika juzi ambao baadhi ya wajumbe wanataka majina yapelekwe, wengine wanapinga.

Katika kikao hicho hoja mbalimbali za kukataa na kukubali kupeleka majina ya makada wanaostahili kuteuliwa zilitolewa kabla kikao hicho hakijaahirishwa bila kuupata mwafaka.

Idadi ya wabunge wa viti maalum hutokana na idadi ya kura walizopigiwa wabunge wote wa chama husika waliosimamishwa majimboni hata kama hawakushinda. Chama kinachopata walau asilimia tano ya kura zote ndicho hukidhi vigezo kutoa majina ya wateule hao.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM ilipata kura milioni 8.3 wa ubunge, Chadema zilikuwa milioni 4.6 na CUF milioni 1.2. Kutokana na kura hizo CCM ilipata viti 64, Chadema 36 na CUF 10.

Idadi ya kura za ubunge zilizopigwa katika uchaguzi mkuu Oktoba 28 hazijawekwa wazi, chama hicho kinafahamu kinastahili kutoa wabunge 22.

Baadhi ya viongozi ndani ya Chadema wanaona ni bora wapeleke orodha hiyo na wabunge hao waende bungeni wakiwa na ajenda mbili ambazo ni kudai tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya.

Kati ya vyama 20 vilivyoshiriki uchaguzi, NEC imevitangaza viwili vyenye sifa ya kupata wabunge wa viti maalumu kwenye Bunge la 12 ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chadema.

Akizungumza na gazeti hili juzi, mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Dk Wilson Mahera hakutaja idadi ya wabunge wa kila chama na kutaka viulizwe vyama husika.

Katika ufafanuzi wake, Dk Mahera alisema vyama hivyo ndivyo vilivyofikisha asilimia tano ya jumla ya kura halali zilizopigwa kwa wagombea ubunge na kwamba tayari CCM kimepeleka majina yake na yamefanyiwa kazi.

Hata hivyo, hadi saa 2:04 assubuhi jana katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika, katika ukurasa wake wa Twitter aliandika kamati kuu haijapendekeza wabunge wa viti maalum.

“Hivyo hakuna orodha iliyopelekwa na katibu mkuu kwa NEC. Tumedokezwa wanataka kughushi saini na orodha Tume ya Taifa ya Uchaguzi ifanye uteuzi haramu na Bunge likabariki,” ameandika Mnyika.

Alipoulizwa kuhusu madai ya Mnyika, Dk Mahera alisema “hilo silijui ila nitaliongelea kesho (leo). Masuala ya uchaguzi yamekwisha, nikienda ofisini nitaangalia kama walichokisema kipo ama la, kesho nitakuwa na nafasi nzuri ya kulisemea.”

Jitihada za kumpata Mnyika ili afafanue suala hilo hazikuzaa matunda kwani simu yake iliita bila majibu lakini kiongozi mmoja wa Chadema alitaka busara itumike katika suala hilo.

“Siasa za Tanzania kwa sasa zinahitaji busara zaidi. Hakuna namna, kukwepa wabunge wasiende bungeni hakutahalalimisha kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.”

“Ni bora wateuliwe wabunge wetu halisi vinginevyo watapelekwa mamluki. Hata ukiwavua uanachama hao mamluki watakimbilia mahakamani,” alisema kiongozi huyo.

Na wakienda mahakamani, kiongozi huyo alisema wanaweza kupata zuio la kutovuliwa ubunge hivyo ni bora chama kikapeleka majina na kuwapa agenda wabunge wake likiwamo suala la Katiba mpya.

“Hakuna Mtanzania asiyejua kilichotokea katika uchaguzi mkuu huu, dunia nzima inajua. Sasa tunasusa katika mazingira yapi? Tuwaache waende ila tuwape ajenda mbili au tatu tu,” alisisitiza.

Katika kikao cha kamati kuu ya Chadema, chanzo chetu kilisema uliibuka mvutano na mgawanyiko huku wajumbe wengi wakitaka chama kipeleke majina.

ACT na baraza la wawakilishi

Jana chama cha ACT Wazalendo kilitangaza msimamo wake kuhusu uteuzi wa wabunge wa viti maalum katika baraza la wawakilishi Zanzibar kwamba hakitoshiriki na kuwataka wananchi kutotegemea kuwaona wabunge hao wakiapishwa.

Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alitoa msimamo huo jijini Dar es Salaam kwenye mkutano na waandishi wa habari alipoeleza tathmini yao ya uchaguzi mkuu na kubainisha yaliyojiri.

Zitto alisema kuna taratibu zinaendelea kufanywa ndani ya chama kwa waliotangazwa kushindwa lakini wananchi wasitegemee kuona wabunge na madiwani waliotokana na chama hicho wakienda kuapa wilayani au bungeni.

“Hakuna jambo muhimu zaidi ya uhai wa watu, sasa hivi siwazi ruzuku, viti maalum wala chochote, ninachowaza ni damu za wanachama zilizomwagika na uhai wa viongozi wangu,” alisema Zitto.

Zitto aliyegombea ubunge Kigoma Mjini alisema hapakuwa na uchaguzi hivyo wajibu wa kulinda haki ni wa wananchi wenyewe.

“Wale waliogombea ubunge na udiwani chama kimewaruhusu kwenda mahakamani lakini kwa nafasi ya urais wananchi ndio mahakama pekee hivyo tutaendelea kupigania haki za wananchi,” alisema.

Katika uchaguzi huo, cha cha ACT kilipata viti vinne vya ubunge hivyo kuwa kushinda viti vingi zaidi. Mwaka 2015, Chadema kilikuwa na wabunge 71 kikifuatiwa na CUF kilichopata 42 wakati ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi vikiambulia mmojammoja.

Nyongeza na Fortune Francis