Waajiri wataja siri za Tanzania kuendelea kupaa zaidi kiuchumi

Waajiri wataja siri za Tanzania kuendelea kupaa zaidi kiuchumi

Muktasari:

Waajiri nchini wamebainisha mambo yanayoweza kuiepusha Tanzania kushuka kiuchumi kutoka nchi ya uchumi wa kati na kuwa na uchumi wa chini kama ilivyotokea kwa baadhi ya mataifa duniani.

Dar es Salaam. Waajiri nchini wamebainisha mambo yanayoweza kuiepusha Tanzania kushuka kiuchumi kutoka nchi ya uchumi wa kati na kuwa na uchumi wa chini kama ilivyotokea kwa baadhi ya mataifa duniani.

Hayo yalibainishwa na waajiri jana jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Chama cha Waajiri nchini (ATE) ambayo ilifunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akiwasilisha mada kwenye hafla hiyo, Mkurugezi mtendaji wa utafiti wa sera ya uchumi na fedha kutoka shirika la Repoa, Dk Donald Mmari alisema baadhi ya nchi duniani ziliingia katika uchumi wa kati lakini baadaye ziliporomoka na kuwa za uchumi wa chini.Alitolea mfano wa nchi za ya Sri Lanka na Sudan.

Hata hivyo, alisema Tanzania inaweza kuepuka kuporomoka kwa kufanya mambo kadhaa ikiwamo kuwekeza kwenye sekta ya kilimo ambayo imeajiri asilimia 65 ya nguvu kazi katika Taifa.

“Sekta ya kilimo itakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa kama tutakiendesha kwa namna tofauti ambayo itakuwa na tija zaidi. Watu wengi wamejiajiri katika sekta hii, kwa hiyo uwekezaji mkubwa ukifanyika kutakuwa na matokeo makubwa,” alisema.

Dk Mmari aligusia pia suala la kuwekeza kwenye sekta ya elimu hasa elimu ya kada ya kati ili wahitimu wawe na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kufanya kazi kwa ufanisi katika ajira zao. Alisisitiza kwamba elimu ya ngazi hiyo ipewe msukumu wa pekee kama ilivyo kwa vyuo vikuu.

Alishauri pia kuitazama upya sekta ya viwanda kwa kuzingatia teknolojia ili Tanzania isiachwe nyuma na mataifa mengine ambayo yanatumia teknolojia ya kisasa katika uzalishaji, jambo linalowafanya watawale kwenye soko.

Jambo jingine, alisema ni kuongeza wigo wa kodi ili Serikali ikusanye mapato ya kutosha sambamba na kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga kama vile ugonjwa wa Covid-19 ambayo yanaweza kuathiri uchumi.

“Ni muhimu kujiandaa kwa majanga ambayo yanaweza kutokea na kuharibu uchumi, mwaka huu tuna Covid-19, tukiwa na viwanda vya dawa hapa nchini, tunaweza kupambana haraka,” alisema Dk Mmari.

Akiwa na mtazamo kama huo, Mtendaji mkuu wa Benki ya Standard Charterd, Sanjay Rughani alisema Taifa linatakiwa kuwa na mkakati wa pamoja wa kiuchumi ili kila mdau ajue mwelekeo wa Taifa kiuchumi.

Aligusia pia sekta ya kilimo akisema inatakiwa kufanyiwa mabadiliko ili iwe na tija badala ya kilimo kufanyika kwa mazoea huku mchango wake ukiwa hafifu katika Pato la Taifa (GDP).

“Tunatakiwa kubadilisha kilimo chetu kutoka kilimo cha mazoea kwenda kilimo cha kisasa. Tukifanya hivyo, tutapata matokeo mara tano zaidi,” alisema Rughani.

Kwa upande wake, Mwakilishi mkazi wa taasisi ya TradeMark East Africa, John Ulanga alisema ili Tanzania ibaki katika uchumi wa kati, lazima pato la Taifa liongezeke zaidi kuliko idadi ya watu na siyo watu waongezeke kuliko pato la Taifa.

“Kuna fursa kubwa kwa Tanzania kuwa katika uchumi wa kati, kwanza tutaaminika na taasisi za fedha, tutavutia uwekezaji na kuboresha huduma za jamii kwa sababu uchumi unakua,” alisema Ulanga.

Akitoa hotuba yake katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwahakikishia waajiri nchini kwamba Serikali itaendelea kufanya nao kazi kwa karibu na tayari imeanza kuboresha mazingira ya biashara hapa nchini.

Alisema Serikali imefuta tozo 168 ambapo kati ya hizo, tozo 114 zimefutwa katika sekta ya kilimo na uvuvi wakati tozo 54 zimefutwa kwenye biashara kwa ujumla.

“Tunaendelea kuisimamia sekta binafsi ili ifanye kazi zake kwa uhuru kabisa na ili itoe mchango katika Pato la Taifa,” alisema Waziri Mkuu na kubainisha kuwa serikali iko tayari kujadiliana na sekta binafsi katika maeneo yenye mgogoro.