Wagombea Eala wajinadi bungeni kwa lugha ya kiingereza

Nadra Mohammed

Muktasari:

  • Wagombea ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala), wameanza kujinadi na kuomba kura mbele ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano Tanzania katika kikao kianchoendelea hivi sasa.


Dar es Salaam. Wagombea ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala), wameanza kujinadi na kuomba kura mbele ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano Tanzania katika kikao kianchoendelea hivi sasa.

Uchaguzi wa kuwapata wabunge hao unafanyika leo Alhamisi Septemba 22, 2022 katika kikao cha Bunge Jijini Dodoma. Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi amesema wagombea hao wataingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kuomba kura kwa kutumia lugha ya kiingereza.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amesema idadi ya kura zitakopigwa kila kundi, akitolea mfano kundi A lina wagombea sita kila unapiga kura tatu, kundi b wagombea wa Zanzibar wapo watano kila mbunge atawapigia wawili.

Dk Tulia amesema kundi C wapinzani ambapo kila mbunge atampigia mgombea mmoja, wakati kundi d linajumuisha wagombea wa Tanzania bara ambao wapo sita na kila mbunge atapiga kura tatu. Kila mgombea anatakiwa kujinadi kwa dakika tatu

Wa kwanza kujinadi alikuwa Angela Kizigha amesema, “nina uwezo wa kutosha wa kusimama na kutetea masilahi ya Taifa katika bunge la Eala. Nataka nikuhakikishe mheshimiwa Spika na wabunge humu nimejidhatiti na nina uwezo wa kulinda maslahi ya Taifa kama kipaumbele changu namba moja.

Aliyefuata ni Nadra Mohammed aliwaomba wabunge kura kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania katika Bunge Eala. Amesema endapo akipata nafasi kipaumbele chake kimojawapo ni kusimamia masilahi ya Taifa.

 “Nitakuwa mstari wa mbele kuhamasisha amani na umoja miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hii. Mheshimiwa Spika na wabunge kwa unyenyekevu naomba kura zenu,” amesema Nadra huku akishangiliwa kwa kupigiwa makofi na wabunge.

Baada ya kumaliza kujinadi mgombea huyo, Dk Tulia aliwauliza wabunge kama wana maswali kwa mgombea huyo, lakini hakukuwa na maswali zaidi ya kuendelea kumpigia makofi na vigeregere.