21 mbaroni wakidaiwa kuua, unyang’anyi wa kutumia silaha

Kamishna wa Polisi Oparesheni na Mafunzo, Awadh Hajji

Muktasari:

Watuhumiwa 21 wa mauaji na unyang'anyi wa kutumia silaha wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika katika matukio ya mauaji na wizi ndani ya Mkoa wa Mara katika kipindi cha mwezi Mei, 2023.

Musoma. Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia watu 21 kwa  tuhuma mbalimbali ikiwemo mauaji na uhalifu wa kutumia silaha katika matukio yaliyotokea mkoani Mara.

Matukio hayo yameelezwa kutokea ndani ya Mwezi Mei mwaka huu na kusababisha vifo pamoja na wizi wa mali hali iliyisababisha kuzuka kwa taharuki juu ya usalama wa wananchi na mali zao mkoani humo.

Takwimu hizo zimetolewa leo Ijumaa, Mei  2023 na Kamishna wa Polisi Oparesheni  na Mafunzo Nchini, Awadh Hajji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo katika kupambana na uhalifu.

Amesema miongoni mwa matukio yanayodaiwa kufanywa  na watu hao ni pamoja na tukio la usiku wa Mei 21, 2023 lililotokea katika kijiji cha Nyankanga wilayani Butiama na kupelekea kifo cha mfanyabishara wa madini ya ujenzi, Nikson Gisiri baada ya kupigwa risasi huku mke wake Mariam Jumanne akijeruhiwa na mtoto mmoja kubakwa.

"Hivi karibuni kumetokea matukio ya kiuhalifu yanayohusu mauaji na unyang'anyi wa kutumia silaha katika mkoa huu wa Mara na mkoa wa kipolisi Tarime/Rora hivyo kuzua hofu na taharuki kwa wakazi wa mkoa juu ya usalma wao pamoja na mali zao,”amesema

Amesema kufuatia matukio hayo ambayo pia yalipelekea  kuuawa kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Nyangoto wilayani Tarime, Dk Isac Sima, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP) alielekeza jeshi hilo kuongeza nguvu na kufanya operesheni mkoani humo ili kuwakamata watuhumiwa wote.

Amesema kufuatia agizo hilo baadhi ya viongozi wa jeshi hilo akiwepo yeye pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) walifika mkoani Mara kwa lengo la kuongeza nguvu.

Kamishna Hajji amesema katika opereheni hiyo waliyoifanya kwa muda mfupi wamefanikiwa kuwakamata watu hao ambao amedai kuwa ni vinara wa matukio hayo ya kiuhalifu na kwamba watuhumiwa hao wamekuwa wakifanya uhalifu wao kwa  kutumia silaha za moto na za jadi.

Ametaja baadhi ya matukio mengine yaliyotokea ndani ya mkoa huo katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na mauaji ya Ramadhan Keryoba (23) mkazi wa kijiji cha Gwiitiryo wilayani Tarime aliyefariki akiwa anapatiwa matibabu hospitalini baada ya kupigwa risasi kichwani alipokuwa dukani kwake kijijini hapo.

"Tukio jingine ni la mauaji ya Otieno Chacha mkazi wa kijiji cha Nyabisaga aliyejeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani  na kuporwa simu aina ya Tecno,”amesema

Amesema jeshi hilo linaendelea na msako ili kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote wanakamatwa huku akiwatoa hofu wakazi wa mkoa huo kuhusu usalama wao.