3000 hufariki kila mwaka nchini kwa kuzama majini

Muktasari:

  • Wakati Watanzania 3000 wakipoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali za kuzama majini, Aprili 2021 Umoja wa Mataifa (UN) uliipitisha Julai 25 ya kila mwaka kuwa siku maalum ya kuzuia kuzama maji duniani kote ( WorldDrowningPreventionDay) inayotarajiwa kuadhimishwa kwa mara kwanza kesho katika fukwe za Kunduchi Beach.

Dar es Salaam. Takribani watu 3000 kila mwaka wanapoteza maisha nchini Tanzania kutokana na ajali za kuzama majini, Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha.

 Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya vifo vya kuzama kwenye maji duniani kote, hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na zile zenye uchumi wa kati.

Akizungumza leo Jumamosi Julai 24, 2021 katika mkutano na vyombo vya habari mkurugenzi mtendaji wa shirika la usimamizi wa mazingira na maendeleo EMEDO, Editrudith Lukanga amesema vifo vya maji vimekuwa vikiua lakini havizungumzwi.

“Kwa Tanzania takribani watu 3000 kila mwaka wanapoteza maisha kutokana na ajali za kuzama majini na vifo hivi ni vingi na hupunguza nguvu kazi ya Taifa,” amesema Lukanga.

Lukanga amesema kwa mujibu wa WHO vifo vya maji ni asilimia 7 ya vifo vyote duniani na hiyo ndiyo sababu wameandaa maadhimisho ya siku maalum ya kuzuia kuzama maji itakayoadhimishwa kwa mara ya kwanza kesho katika fukwe za Kunduchi.

“Takribani watu 236,000 duniani kote hupoteza maisha kutokana na ajali za maji," amesema Lukanga.

Diwani wa Kata ya Kunduchi, Maiko Urio amesema ajali za majini zimekuwa zikitokea zaidi maeneo ya fukwe za bahari na maziwa makuu na baadhi ya watu huonekana na wengine hupotea kabisa huku kundi la wavuvi likitajwa kuathika zaidi.

"Kwa mwaka huu peke yake mimi nimehudhuria mazishi ya wavuvi watatu katika kata yangu ya Kunduchi. Hii ni Kunduchi peke yake bado hujakwenda Kigamboni, Tanga, Mafia na kwingineko. Vifo ni vingi, tunahitaji nguvu moja,"  amesema Urio.

Aprili 2021 Umoja wa Mataifa (UN) iliipitisha Julai 25 ya kila mwaka kuwa siku maalum ya kuzuia kuzama maji Duniani kote ( WorldDrowningPreventionDay) lengo ni kukutana, kujenga uelewa wa pamoja juu ya athari za ajali za kuzama kwenye maji na kuweka mikakati ya kudhibiti ajali hizo.