Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

32 wakosa makazi, moto ukiteketeza makazi

Baadhi ya mali zilizoteketea kwa moto Rombo

Muktasari:

  • Moto huo ulioteketeza vyumba 11, vikiwa na vyakula, malazi na fedha umesababisha familia za watu 32 kukosa mahali pa kuishi, huku baadhi ya wanafunzi wakishindwa kwenda shule baada ya sare zao za shule kuteketea kwa moto.

Rombo. Kaya saba katika Kijiji cha Mbomai, Kata ya Tarakea Motamburu, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi yenye vyumba 11 kuteketea kwa moto.

Tukio hilo la moto, lilitokea jana Februari 6 usiku saa 1:30 na kuteketeza mali zote zilizokuwepo kwenye vyumba hivyo zikiwemo fedha, vyakula na mavazi huku chanzo chake kikiwa bado hakijajulikana.

Akizungumzia tukio hilo la moto, Mwenyekiti wa kijiji cha Mbomai, Andrea Sarita amesema eneo la mji wa Tarakea limekuwa likikumbwa na majanga mengi ya moto na wanashindwa kuyadhibiti kutokana na kwamba kwenye eneo hilo hakuna gari la zimamoto.

"Suala la majanga ya moto katika eneo hili la Tarakea limekuwa likitokea mara nyingi na kugharimu maisha ya watu pamoja na mali zao, kutokana na kwamba eneo hili halina gari la zimamoto na wakati mwingine tunasaidiwa na majirani zetu wa Kenya.

"Tunawaomba viongozi wetu wa Serikali waone sasa maneno haya hata kama wilaya yetu haina gari waangalie njia mbadala tupate gari hata moja la zimamoto ndani ya wilaya maana hapa Tarakea hatuna gari licha ya kwamba mji huu unakuwa kwa kasi," amesema.

Naye Diwani wa Kata ya Tarakea Motamburu, Felichism Oisso amesema mpaka sasa familia hizo hazina mahali pa kuishi na kwamba wameshatoa taarifa kwenye mamlaka zinazohusika ili kuzisaidia familia hizo.

"Kaya zote 7 hazina mahali pakwenda baada ya vyumba vyao na mali zao zote kuteketea kwa moto, hawa watu hawana msaada wowote na mpaka sasa hawana chakula maana vyakula vyao na fedha zao zote zimeteketea kwa moto," amesema.

Amesema mji wa Tarakea licha ya kwamba unakuwa kwa kasi hauna gari la zimamoto na suala la mipango miji limekuwa ni tatizo kubwa sana katika mji huo.

"Tunachokifanya kwa sasa ni kuzungumza na watu ambao wana moyo wa kusaidia ili kuweza kuwahifadhi watu hawa kwa muda wakati tukisubiria mambo mengine maana tumeshatoa taarifa kwenye mamlaka zinazohusika kuona namna ya kutusaidia ili watu hawa waweze kupata chakula na mavazi na sehemu ya kujihifadhi kwa muda,"

Naye Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM, ngazi ya mkoa, Godfrey Mwaiyo amesema  kutokuwepo kwa mipango miji katika mji huo  ni moja ya changamoto ya kuwepo kwa matukio ya majanga ya moto ambayo hayadhibitiki kutokana na mpangilio uliopo kwa sasa.

"Sisi kama cha Mapinduzi tunatoa pole kwa familia hizi, lakini tuziombe mamlaka za serikali katika wilaya hii kwa namna yoyote waangalie namna ya kuwasadia wananchi hawa kwa sasa,"

Selina Frank, ambaye ni mmoja wa waathirika wa tukio hilo amesema wakati moto huo ukitokea hakuwepo nyumbani na aliporudi kwenye shuguli zake za kila siku alikuta kila kitu kimeteketea kwa moto.

"Sina hata kimoja nilichoweza kukiokoa, vyakula vilivyokuwepo ndani, nguo pamoja na fedha zilizokuwepo ndani zote zimeteketea kwa moto, hapa nipo tuu na nguo nilizokuwa nimevaa jana na watoto hawana hata nguo za shule, tumebaki hatuna chochote, tunaomba serikali itusaidie,"

Halifa Amiri, ambaye fedha zake zaidi ya Sh1.5milioni, vyakula na mavazi vimeteketea kwa moto ameiomba serikali kuona namna ya kuwasadia kutokana na kwamba hawana makazi na wanalazimika kulala nje.

"Mpaka sasa tunalala nje maana hatuna chochote tulicho nacho, tunaomba serikali iangalie namna ya kutusaidia maana mali zote tulizokuwa nazo ndani zote zimeteketea kwa moto, na hata hawa watoto hatujui wanaenda shule mpaka sasa," amesema.