67 mbaroni Pwani kwa tuhuma za wizi, biashara haramu

Muktasari:

  • Msako wa wiki mbili mkoani Kibaha, umefanikisha kukamata watu 67 waliokutwa na mali zinazodaiwa kuwa za wizi pamoja na tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ikiwemo pombe haramu.

Kibaha. Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani linawashikilia watu 67 kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo wizi na kujihusisha na biashara haramu.

 Baadhi ya mali wanazodaiwa kukutwa nazo watuhumiwa hao ni pamoja na pikipiki 10, silaha moja aina ya gobole, pombe ya moshi lita 13 na viroba vitatu vya bangi, puli 102 na kete 789 na dawa hizo haramu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Machi 14, 2023 Kamanda wa Polisi mkoani Pwani,   Piusi Lutumo amesema kuwa msako huo uliofanyika kwa wiki mbili na mafanikio yake yametokana na ushirikiano mzuri kutoka kwa raia wema.

"Tumefanya msako kwa wiki mbili na tumefanikiwa na hii inatokana na ushirikiano mzuri baina yetu na wasamalia wema kwa kutupatia taarifa za siri," amesema Kamanda Lutumo.

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi hilo zinazohusiana na vitendo vya uharifu Ili watu hao wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.