Abiria wapewa mbinu kuepuka kulanguliwa tiketi mabasi mkoani
Muktasari:
- Wamiliki wa mabasi mkoani Iringa watakiwa kutumia mfumo wa tiketi mtandao kudhibiti vishoka na wapiga debe wanaolangua tiketi msimu wa sikukuu na kuziuza kwa gharama ya juu.
Iringa. Wamiliki wa mabasi mkoani Iringa wametakiwa kutumia mfumo wa tiketi za mtandao ili kudhibiti matapeli na vishoka ambao wamekuwa wakifanya ulanguzi wa tiketi na kupandisha nauli kiholela kinyume na sheria za usafirishaji hususani kipindi cha sikukuu na kusababisha abiria kununua tiketi mara mbili ya bei elekezi ya serikali.
Mfumo huu wa kukata tiketi kwa njia ya mtandao unamuwezesha msafiri kukata tiketi kwakutumia simu yake ya mkononi bila kulazimika kufika katika ofisi za mabasi kufuta huduma hiyo.
Hayo yamesemwa leo Machi 18, 2023 na baadhi ya wamiliki wa mabasi mkoani Iringa wakati wakipewa elimu ya tiketi za mtandao inayotolewa na Mamlaka ya Mapato TRA mkoani hapo.
Baadhi ya wamiliki wa mabasi mkoani hapa wanasema mfumo huo utasaidia kudhibiti mianya ya rushwa iliyokuwa ikipelekea kupata hasara kutokana na vishoka na walanguzi wa nauli.
Akuzungumza Mkurugenzi wa Kampuni ya Upendo Coach inayofanya safari zake kati ya Iringa na Dar es Salaam, Charles Nyagawa ameipongeza Serikali kwa kuja na mfumo huo akisema utawasaidia kwa kiwango kikubwa kuyanusuru mapato yao yaliyokuwa yakichotwa na wapiga debe.
“Kuna wakati mpigadebe anamkatia tiketi abiria kwa Sh25,000 kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam lakini kwa kisingizio kwamba yeye ndiye kamtafuta abiria huyo anachukua Sh7,000 mmiliki anaachiwa Sh 18,000,” amesema.
Nyagawa amesema kuwa kimahesabu kiwango hicho ni kikubwa na kinampa maumivu mmiliki kwasababu mbali na kulipa kodi mbalimbali za Serikali kwa kutoa huduma hiyo ya usafirishaji, anatakiwa kuwalipa wafanyakazi, mafuta na matengenezo ya basi lenyewe.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Shabani Salim amesema ili mpango huo ulioanza kutekelezwa Julai mwaka jana ufanikiwe mamlaka yao inaendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa mabasi.
“Leo tumekutana hapa Iringa na wamiliki wa mabasi ya abiria waliopo mkoani kwetu Iringa kwa lengo lilelile la kufikisha zaidi elimu kuhusu mfumo huu, jinsi unavyofanya kazi na faida zake ikiwemo serikali kupata mapato yake sahihi,” amesema.
Amesema wapo watoa huduma wachache waliounganisha mfumo wao na TRA na kwa ambao bado wanatakiwa kujiunga ili taarifa zote za tiketi zinazokatwa zionekane katika mamlaka hiyo kwa lengo la kufuatilia mapato yanayotokana na huduma ya usafirishaji.
Kwa upande wake Meneja wa Tiketi Mtandao kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Thadei Mwita alisema tiketi mtandao zinafaida kubwa kwa wamiliki wa mabasi kwani zinawanusuru na upotevu wa fedha zinazochukuliwa na wapiga debe kwa kisingizio cha kutafuta abiria.
“Mfumo huo wa tiketi mtandao umewasaidia kwa kiasi kikubwa wamiliki wa mabasi na kuzuia mianya ya upotevu wa mapato pamoja na fedha ambazo walipaswa kupata wao lakini awali ziliku zikienda moja kwa moja kwa wapiga debe,” amesema.
Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) Mkoa wa Iringa, Mohamed Ally ameishukuru TRA kwa kuwashirikishwa kwenye kikao hicho na akasisitiza suala la utoaji wa elimu kuhusu tiketi mtandao kwa watumiaji, lakini pia kwa baadhi ya wasafirishaji ambao bado hawajaanza kutoa huduma hiyo ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.
“Mfumo wa Tiketi Mtandao una umuhimu na faida kubwa ikiwemo kuokoa muda ambao abiria anatumia wakati wa kwenda kukata tiketi katika ofisi za mabasi, kuepuka changamoto za wapiga debe. Pia husaidia abiria kupata stahiki zake endapo itatokea ajali au madhara yoyote kwa kupewa fidia na bima,” amesema.