ACT-Wazalendo yajitwisha zigo ujenzi wa soko Kibondo

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akiteta jambo na mmoja wa wajasiriamali wa mazao ya samaki katika Soko la Samaki mjini Kibondo wakati alipotembelea soko hilo kujionea miundombinu na mazingira ya biashara. Zitto ameahidi kutafuta Sh200 milioni kutoka kwa wafadhili mbalimbali kuboresha miundombinu ya soko hilo. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Jimbo la Muhambwe, Nicholaus Kilunga. Picha na Sunday George.

Muktasari:

Soko la Samaki linategemewa na wafanyabiashara zaidi ya 300 wanaouza bidhaa mbalimbali ikiwemo mbogamboga, mazao ya samaki na nafaka. Awali eneo lilipo soko hilo lilitengwa kuwa eneo la wazi kabla ya watu kuanza kulitumia kama sehemu ya kuuza na kununua bidhaa; hali ambayo sasa imeilazimisha Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kuanza mchakato wa kulibadilishia matumizi kutoka eneo la wazi kwenda eneo la kibiashara.

Kibondo. Chama cha ACT-Wazalendo kimeahidi kutafuta zaidi ya Sh200 milioni kwa ajili ya moboresho ya miundombinu ya Soko la Samaki mjini Kibondo.

Ahadi hiyo imetolewa Novemba 17, 2023 na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe wakati wa mkutano wa hadhara mjini Kibondo baada ya kutembelea soko hilo linalotumiwa zaidi ya wajasiriamali zaidi ya 300 wanaouza bidhaa mbalimbali za chakula.

‘’Nimetembelea Soko la Samaki, nimeona miundombinu duni ambayo  wafanyabiashara wanafanyia kazi, hakuna miundombinu ya majitaka, hakuna paa la kuwakinga wafanyabiashara; mvua likija ni lao na mvua pia lao. ACT-Wazalendo tutatafuta fedha kujenga miundombinu ya soko lile,’’ amesema Zitto

Amesema kwa hesabu za haraka, maboresho ya miundombinu ya soko hilo inaweza kugharimu zaidi ya Sh200 milioni, gharama ninayoamini iko ndani ya uwezo wa halmashauri nia ikiwepo.

‘’Sisi ACT-Wazalendo tutazungumza na wafadhili mbalimbali kutafuta fedha na kuzileta hapa Kibondo kuboresha miundombinu ya soko lile tuone kama halmashauri watazikataa kwa sababu zimeletwa na Zitto,’’ amesema kiongozi huyo

Amesema uamuzi wa kutafuta fedha za kuboresha miundombinu ya soko hilo unalenga siyo tu kuweka mazingira bora kwa wajasiriamali, bali pia kulinda afya za wana Kibondo wanaotegemea soko hilo kwa mahitaji ya msingi ya vyakula kuanzia mbogamboga, mazao ya samaki na nafaka.

Awali, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo jimbo la Muhambwe, Nicolas Kilunga alimweleza Zitto kuwa uduni wa miundombinu katika maeneo ya biashara ni miongoni mwa kero wanazokumbana nazo wajasiriamali licha ya kulipa ushuru kwa halmashauri.

Mipango ya halmashauri

Akizungumzia kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Deocres Rutema, Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Adam Mapunda amesema halmashauri hiyo tayari imeweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya soko hilo itakayogharimu zaidi ya Sh350 milioni.

‘’Mradi huu utatekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza itakayotekelezwa mwaka wa fedha wa 2024/25 itagharimu Sh150 milioni, awamu ya pili itakayotekelezwa mwaka wa fedha wa 2025/6 itagharimu Sh100 milioni, sawa awamu ya mwisho ya mwaka wa fedha 2026/27 itakayogharimu Sh100 milioni’’ amesema Mapunda

Ametaja baadhi ya shughuli zitakazofanyika katika maboresho hayo kuwa ni ujenzi wa vibanda vya biashara, kibanda au jengo kuu la katikati lenye paa kwa ajili ya kuwakinga wafanyabiashara dhidi ya jua na mvua na maeneo mengine muhimu kwa shughuli za kibiashara ikiwemo maegesho ya magari.

Kubadili matumizi

Ili kufanikisha lengo hilo, Ofisa Mipango huyo amesema halmashauri imelazimika kubadilisha matumizi ya eneo lilipo soko hilo kutoka eneo la wazi kuwa eneo la kibiashara.

‘’Kwa mujibu wa mipango miji, eneo lilipo Soko la Samaki ni eneo la wazi; hivi sasa tunatekeleza mchakato wa kubadilisha matumizi yake kutoka eneo la wazi kwenda eneo la biashara kabla ya kutekeleza mradi wa maboresho ya miundombinu yake,’’ amesema Mapunda

Amesema tayari halmashauri imewasilisha mapendekezo na ramani kwa Kamishina wa ardhi kuomba eneo hilo libadilishwe kutoka la wazi kuwa la kibiashara, mpango anaoamini utakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

‘’Ni matumaini yetu kuwa Kamishina wa Ardhi atapitisha mabadiliko ya eneo lile kutoka eneo la wazi kuwa eneo la kibiashara ifikapo Desemba, 2023 ili kutuwezesha halmashauri kuendelea na mipango ya maboresho ya miundombinu ya soko,’’ amesema Mapunda

Wajasiriamali watoa neno

Magdalena Simon, mjasiriamali wa mbogamboga Soko la Samaki Kibondo ameupongeza uongozi wa ACT-Wazalendo kwa kuonyesha kuguswa na tatizo la muda mrefu la mazingira duni ya biashara eneo hilo huku akiomba mipango ya kutafuta fedha za kurekebisha hali hiyo iharakishwe.

‘’Tumemsikia Zitto akiahidi kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili kusaidia ujenzi wa soko letu, huu utakuwa ukombozi kwetu na wateja wetu na tunamwombea Mungu amwezeshe kutimiza lengo hilo mapema,’’ amesema Magdalena

Kauli hiyo imeungwa mkono na Hamisi Ramadhani, mjasiriamali wa nafaka huku akiuomba utekelezaji wa mradi huo kwa fedha kutoka ACT-Wazalendo liangaliwe kwa macho ya kuhudumia jamii badala siasa.

‘’Nausihi uongozi wa ACT-Wazalendo na halmashauri washirikiane katika mpango wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya Soko la Samaki bila kujali masuala ya kisiasa kwa maslahi na faida ya jamii sababu maendeleo hayacha chama,’’ amesema Ramadhani