ACT Wazalendo yatoa mapendekezo Wizara ya Habari

Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari, Philbert Macheyeki

Muktasari:

Mei 19, 2023, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliwasilisha taarifa Bungeni ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/23 na Mpango wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambapo Bunge lilijadili na kupitisha bajeti ya wizara hiyo Sh212.5 bilioni.

Mwanza. Chama cha ACT Wazalendo kimetoa mapendekezo saba kufuatia taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/23 na mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari, Philbert Macheyeki imeitaka Serikali kufuta sheria zote kandamizi zinazopora uhuru wa vyombo vya habari na kutengeneza sheria mpya kwa kushirikiana na wadau ambazo zitaleta uhuru, weledi na ukuaji wa sekta ya habari.

Macheyeki amesema Serikali isimamie uanzishwaji wa baraza huru la habari nchini ili kulinda na kutetea haki na maslahi ya wanahabari huku akiitaka kuongeza ushirikishwaji katika mchakato wa mapitio ya sheria ya huduma ya habari na muswada uliowasilishwa Bungeni Februari, 2023 upelekwe kwa wadau kujadiliwa kwa kina.

“Tunaitaka Serikali kufanya marekebisho ya kanuni zinazosimamia vifurushi vya dakika za kupiga miongoni mwa mitandao nchini, bando ya intaneti na meseji kwa kuwashirikisha vyakutosha wananchi ili kuwezesha kudhibiti, uholela wa makampuni kuamua na kuwa na gharama nafuu,”amesema

Ametaka uanzishwe mchakato wa kutengeneza upya sera ya taifa ya mawasiliano kwa kuwashirikisha kikamilifu watoa huduma, watumia huduma, wataalamu wa masuala ya kimtandao na wadau wengine ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani.

Amesema serikali Ihakikishe inatatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano na mitandao ya simu za mikononi katika maeneo ya vijiji ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

“kwa mujibu wa taarifa ya uchambuzi ya wizara ya mwaka 2022 ambayo imetumika katika bajeti hii ya 2023/24 asilimia 69 ya ardhi ya Tanzania imefikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu za kiganjani ikilinganishwa na asilimia 66 ya mwaka 2021,

“Kwa maana nyingine wastani wa wananchi asilimia 31 hawapati huduma ya mtandao wa simu. Aidha takwimu zinaonyesha kuna zaidi ya vijiji 2, 212 vina changamoto ya mawasiliano nchini mpaka kufikia Aprili, 2023 huku vijiji 616 tu ndio vilifikiwa na huduma ya mawasiliano kwa kujengewa minara kwa mwaka wa fedha uliokwisha,”amesema

Amependekeza Serikali itoe huduma ya data bure katika maeneo yote ya umma zikiwemo hospitali, shuleni, vyuoni, maofisini na sokoni.

“Hata hivyo katika kuelekea kwenye mabadiliko makubwa ya kidigitali mchango wa sekta ya habari ni mkubwa sana kwahiyo ipo haja ya serikali kuwekeza vya kutosha ili kuhakikisha inaboresha miundombinu ya mawasiliano inakuwa vizuri ili kuboresha na kuimarisha uchumi wetu,”