Ada-Tadea yataka Tume huru kabla ya 2025

Mwenyekiti Chama cha Ada-Tadea, John Shibuda

Muktasari:

Chama cha Ada-Tadea kimeshauri upatikanaji wa Tume huru ya Uchaguzi kabla uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na ule mkuu 2025.

Dar es Salaam. Chama cha Ada-Tadea kimeshauri upatikanaji wa Tume huru ya Uchaguzi kabla uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na ule mkuu 2025.

Chama hicho ni miongoni mwa vyama vinne vinavyotoa maoni yake mbele kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia nchini. Vyama vingine ni UPDP, AFP na ADC.

Akizungumza leo Jumatano Mei 25, 2022 baada ya kuwasilisha maoni, Mwenyekiti wa chama hicho, John Shibuda amesema chama hicho kimewasilisha mapendekezo katika maeneo yote tisa ikiwamo suala la tume hiyo inayohitajika mapema.

“Tume itazamwe upya teuzi zake, kuwepo na maboresho yatakayojenga imani kwa wananchi na wadau wa siasa, ambao wataona kwamba tume hii sasa inakuwa wasimamizi wanaotekeleza majukumu yao kwa uhuru,” amesema.

“Kwa sababu maandalizi ya tume huru haihitaji pesa nyingi kama masuala ya Katiba, basi ni muhimu marekebisho haya yafanyike haraka iwezekanavyo kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa na ule uchaguzi mkuu 2025.”

Kuhusu hoja ya katiba, mwenyekiti huyo wa zamani wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini amesema ni muhimu kufanyia marekebisho ya andiko jipya la katiba badala ya kuendelea na katiba pendekezwa au iliyopo sasa.