Adaiwa kukutwa na bangi kituo cha kupigia kura

Adaiwa kukutwa na bangi kituo cha kupigia kura

Muktasari:

  • Juma Hamad Saleh (19) mkazi wa Msuka Konde amekamatwa akiwa na bangi katika kituo cha kupigia kura Jimbo la Konde.

  

Pemba. Juma Hamad Saleh (19) mkazi wa Msuka Konde amekamatwa akidaiwa kuwa na bangi katika kituo cha kupigia kura Jimbo la Konde.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Sadi Khamis amesema tukio hilo limetokea leo Jumamosi Oktoba 9, 2021 katika kituo cha kupigia kura cha Msuka Magharibi.

Kamanda Khamisi amesema kijana huyo alitiliwa mashaka na alipopekuliwa akakutwa na misokoto minne ya bangi.

"Yule kijana alifika mara ya kwanza akaondoka bila kupiga kura kisha akarudi mara ya pili lakini akatiliwa shaka ndipo alikamatwa na kuanza kupekuliwa akakutwa na nyongo (misokoto) nne za bangi," amesema Kamanda Khamis.

Hata hivyo, Kamanda Khamis amesema hali ya usalama ni shwari, bado hakujatokea tukio lolote la kuashiria uvunjifu wa amani ukiachilia mbali tukio hilo la bangi.

"Nimeshazungukia vituo vyote vya uchaguzi, hali ni shwari  wananchi wamejitokeza kupiga kura kumchagua kiongozi wao," amesema.

Amesema Jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha hali hiyo ya utulivu na amani inaendelea kutawala katika kipindi chote cha mchakato huo wa uchaguzi mpaka atakapotangazwa mshindi.

Kwa mujibu wa Khamis mtu yeyote atakayejaribu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu.

Jumla ya vyama vinne vimesimamisha wagombea ambavyo ni Chama cha Wakulima (AAFP), Chama Cha Wananchi (CUF), ACT- Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Uchaguzi huu umefanyika kutokana na aliyechaguliwa Julai 18 mwaka huu, Sheha Faki Mpemba (CCM), kujiuzulu kabla ya kuapishwa kwa madai ya kutishiwa maisha na watu aliowaita wapinzani wake.