Adaiwa kumuua baba na dada yake kwa kuwachoma visu, naye apoteza maisha

Sunday January 17 2021
Auwa baba, dada pic
By Jesse Mikofu

Mwanza. Richmond Kalenga (32) anadaiwa kuwaua baba na dada yake  kwa kuwachoma visu wakiwa nyumbani kwao Mtaa wa Nyashana B Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Waliouawa na ndugu huyo ni Benedicto Franabo (66) ambaye ni baba na Renata Benedicto (42) dada wa kijana huyo.

Kamanda wa polisi wa Mkoa huo, Jumanne Muliro amesema leo Jumapili Januari 16, 2020 kwamba tukio hilo lilitokea Januari 15 saa tisa alasiri.

Hata hivyo, kamanda Muliro amesema baada ya kijana huyo kutenda tukio hilo, alishambuliwa na wananchi waliofika nyumbani hapo kutoa msaada ambapo nayeye alifariki akiwa njiani akikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekoutoure.

"Kwanza alimchoma visu baba wake katika maeneo mbalimbali ya mwili wake,  akamfuata dada yake naye akamchoma visu na kuwasababishia umauti," aliongeza Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amesema baada ya kutenda tukio hilo majirani walikusanyika kutoa msaada lakini alianza kuwarushia mawe, hata hivyo walifanikiwa kumdhibiti na kuanza kumshambulia kabla ya polisi kufika na kumkuta akiwa katika hali mbaya na kumkimbiza hospitalini, ambako hakufika kwani alipoteza maisha akiwa njiani.

Advertisement

Kwa mujibu wa kamanda Muliro, taarifa za awali kijana huyo alikuwa anasoma Chuo Kikuu cha Kampala Gongo la Mboto ambapo aliacha shule na kurejea nyumbani akawa anaishi na baba na dada wake.

Hata hivyo amesema tangu arejee nyumbani (haikujulikana ni lini) lakini hakuwa na mahusiano mazuri na familia yake.

Kwa ufupi

Adaiwa kuua baba na dada wake kisha na yeye kupoteza maisha kwa kushambuliwa na wananchi.

Advertisement