Afariki dunia akidaiwa kuchomwa visu

Amina Hassan

Muktasari:

Mtoto wa marehemu (jina linahifadhiwa) aliyedai kushuhudia tukio hilo, amesema kuwa wazazi wake walikua wakigombana usiku, baba yake alipotoa kisu kwenye mfuko na kuanza kumchoma mama yake.

Geita. Mkazi wa Lukirini, Kata ya Kalangalala, wilayani hapa, Amina Hassan amefariki dunia wakati anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Geita baada ya kudaiwa kuchomwa kitu chenye ncha kali na mumewe.

 Mganga mfawidhi hospitali ya mkoa wa Geita, Dk Mfaume Salum amethibitisha kutokea kwa kifo hicho ambapo amesema Agosti 31, 2022 saa sita usiku walimpokea Amina akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali.

Amesema mama huyo alikuwa na majeraha maeneo ya mgongoni, kifuani na tumboni yaliyoleta madhara kwenye viungo vilivyoko ndani ya tumbo na kifuani na kufanyiwa upasuaji usiku huohuo na na alipotoka kwenye chumba cha upasuaji alipoteza maisha.

"Mama huyu baada ya kupokelewa alikua anamajeraha sehemu za mwili hasa tumboni na tulibaini yameleta madhara katika viungo vilivyoko ndani ya tumbo tulimfanyia upasuaji usiku huo huo na baada ya kutoka kwenye chumba cha upasuaji baada ya masaa 20 alifariki," amesema Dk Salum.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ally Kitumbu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema chanzo ni mgogoro wa kifamilia kati ya marehemu na mumewe.

Amemtaja mwanaume huyo kuwa ni Mashaka Jeremia ambaye ni mchimbaji wa dhahabu na mkazi wa Lukirini anaedaiwa kutoroka baada ya kufanya ukatili huo.

Amesema wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa wa Geita.

Mtoto wa marehemu (jina linahifadhiwa) ambaye nu mwanafunzi wa shule ya sekondari Mujumuzi amesema alishuhudia, ambapo wazazi wake walikua wakigombana usiku na baba yake kuanza kumpiga kisha kutoa kisu kwenye mfuko na kuanza kumchoma mama yake na kumsababishia majeraha makubwa.

Amesema wakati baba yake akiendea kumchoma kisu mama yake alifungua dirisha kuomba msaada ndipo baba alipomuacha na kufungua mlango kisha kukimbia.