Afariki saluni akisubiri kunyolewa
Muktasari:
- Mkazi wa kijiji cha Roselini, Kata ya Indumet, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Godfrey Bange amefariki dunia akiwa saluni akisubiri kunyolewa.
Siha. Mkazi wa kijiji cha Roselini, Kata ya Indumet, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Godfrey Bange amefariki dunia akiwa saluni akisubiri kunyolewa.
Tukio hilo, lilitokea Julai 10, mwaka huu wakati mwanaume huyo akiwa amekaa kwenye sofa katika moja ya saluni zilizopo katika kijiji cha Ngarenairobi wilayani humo akisubiri kunyolewa baada ya kukuta foleni kubwa.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Siha ambaye pia ndiye Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Timbuka ameiambia Mwananchi Digital kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
“Ni kweli, tukio hilo limetokea kama ulivyoelezwa, na kwa mujibu wa vipimo vya kitabibu, marehemu Bange alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu. Ni kifo cha kaiwaida kisichotiliwa shaka,” amesema.
Akisimulia tukio hilo, mmiliki wa saluni hiyo, Seleman Mfaume amesema mwanaume huyo alipofika saluni hapo muda wa mchana na kukuta kuna foleni kubwa na kwamba alimuomba mteja wake huyo kusubiri kidogo.
Kwa mujibu wa Mfaume, wakati mteja huyo anasubiri kunyolewa, muda wa kuswali ulikuwa umeshawadia, hivyo kwa sababu mteja wake (marehemu) alikuwa amelala kwenye sofa, akaamua kwenda msikitini kwanza na kwamba atakaporudi basi angemnyoa.
"Wakati natoka msikitini kuswali nilimwamsha ili nimnyoe lakini hakuamka, nikamwomba mteja mwingine aliyekuwepo saloon hapa anisaidie na yeye kumtikisa tikisa ili aamke nimnyoe lakini hakuamka jambo ambalo lilitushtua kidogo," amesema Mfaume.
Baada ya jitihada za kuamsha kushindikana, mmiliki huyo wa saluni alilazimika kumtafuta Mtendaji wa eneo hilo, na hata mtendaji alipofika saluni hapo, naye alijaribu kumuamsha bila mafanikio, na kwamba mwili mteja huyo ulionyesha dalili za kupoa.
Taarifa zinasema kuwa walifanya jitihada za kutafuta gari kumpeleka hospitali ya jirani na alipofikishwa hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo alibainika kuwa amekwishafariki.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mtendaji wa kijiji cha Ngarenairobi, Seif Mwamgamba, ambaye alikuwepo kwenye eneo la tukio, amesema tukio hilo limetokea wakati mwanaume huyo akiwa kwenye foleni akisubiri kunyolewa.
"Baada ya kupigiwa simu na kufika saluni hapo tulifanya jitihada za kumwamsha bila mafanikio, tayari mwili wake ulikuwa umeshapoa, hivyo tulifanya jitihada za kutafuta gari kumpeka hospitali ya Kibong'oto na baada ya kupokelewa madaktari walithibitisha kuwa ameshafariki," amesema Mtendaji huyo.