Afrika kujadili athari mabadiliko ya tabia nchi sekta ya afya

Muktasari:

  • Viongozi wa kisiasa, watunga sera, mashirika ya kiraia, wadau sekta ya afya na viongozi wa hali ya hewa wanatarajiwa kukutana jijini Kigali, Rwanda Machi mwaka huu kujadili sera za afya za Afrika dhidi ya changamoto za kimataifa, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, uhaba wa chakula, migogoro na mdororo wa kiuchumi.

Dar es Salaam. Wadau wa afya na maendeleo kote duniani wanatarajia kukutana katika Mkutano wa tano wa Kimataifa wa Ajenda ya Afya Afrika (AHAIC) utakaofanyika Machi 5-8, 2023 jijini Kigali nchini Rwanda.

 Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, utajikita kuzungumzia mambo anuai ajenda kuu ikiwa ni mabadiliko ya tabia nchi ikiangazia mifumo stahimilivu ya afya kwa Afrika na kutafakari upya mustakabali wa sasa.

Mkutano huo ulioitishwa kwa pamoja na Amref Health Africa, Wizara ya Afya Rwanda, Umoja wa Afrika na vituo vya afrika vya kudhibiti na kuzuia magonjwa (Africa CDC), utawaleta pamoja viongozi wakuu wa fikra za bara hilo, wanasiasa, wavumbuzi, watafiti, watunga sera na asasi za kiraia kwa mazungumzo na hatua zinazolenga kuingiza mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi na sera ya afya.

"Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mkutano wa kimataifa wa afya barani Afrika kuangazia mabadiliko ya tabia nchi kama kigezo muhimu cha afya.

“Tunajua kwamba mabadiliko ya tabia nchi na afya vimeingiliana, hata hivyo kwa miongo kadhaa sasa yamechukuliwa kama masuala mawili tofauti,” alisema Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Amref Health Africa Dk Githinji Gitahi.

Dk Gitahi alisema mkutano wa mwaka huu utakuwa ukichunguza mada katika uhusiano wa mabadiliko ya tabia nchi na afya ikijumuisha sayari inayoongezeka kwa kasi ya joto, kujiandaa kwa janga, usalama wa chakula na lishe, uvumbuzi, utafiti na maendeleo, jinsia na migogoro.

AHAIC 2023 inakuja katika msingi wa wito mpya wa viongozi wa Afrika wa kuchukua hatua za haraka zaidi dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi wakati athari zake zikiendelea kuonekana ambapo kutakuwa na vikao vilivyoratibiwa kupata suluhisho endelevu na shirikishi.

"Mataifa ya Afrika yanasalia katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi. Tayari tunahisi madhara ya kudhorota kwa afya duniani kutokana na hali mbaya ya hewa na ukosefu wa usalama wa chakula, upatikanaji mdogo wa maji safi na magonjwa ya milipuko ya mara kwa mara.

“Hata hivyo masuala haya yamesalia pembezoni, mazungumzo licha ya kuwepo kwa ushahidi wa kisayansi kwamba mabadiliko ya tabia nchi yanatishia ustawi wetu," alisema Waziri wa Afya Rwanda, Dk Sabin Nsanzimana.

Wakati dunia inakaribia kufikia 2030 ambapo ndiyo mwisho ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, viongozi wa Afrika katika mkutano huo watakuwa wakihimiza jumuiya ya kimataifa kufanya upya ahadi zake za kukomesha umaskini na kuboresha afya na ustawi na wakati huo huo kulinda sayari.

Huku kukiwa na idadi ya vijana wakifikia bilioni 1.2 ambao wana uwezekano wa kubeba mzigo mkubwa wa mabadiliko ya hali ya hewa, washiriki katika mkutano huo pia watakuwa wakitetea rasilimali zaidi kutengwa ili kutatua shida za afya na mabadiliko ya tabia nchi wakati tukiondoka katika miaka mitatu ya Uviko19.

"Wakati tunabakia kuwa na matumaini juu ya uwezo wa dunia kuzuia na kuhimili janga linalofuata, lazima pia tutambue kuwa hatuwezi kuishi kile ambacho hatujitayarishi. Ni muhimu tuungane pamoja ili kutafuta suluhu za changamoto za leo na za kesho tukiwa bado na fursa,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mkuu Afrika CDC, Dk Ahmed Ogwell Ouma.

AHAIC 2023 inalenga kuunda msimamo wa pamoja wa Afrika kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kabla ya mazungumzo muhimu yatakayofanyika katika Mkutano wa Afya wa Dunia, kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 78) na kikao cha 28 cha Mkutano wa Umoja wa Mataifa (COP 28) baadaye mwaka huu.

Mkutano huo utaanza na mbio za marathon (AHAIC 2023 Wogging Marathon) Machi 5 ikifuatiwa na siku tatu za kikao, mikutano ya viongozi, warsha na vikao vya mitandao ambavyo vitafanyika kuanzia Machi 6 hadi 8.