Agizo la Rais Samia lamuibua RC Mongella

Tuesday September 14 2021
arushaapicccc

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella

By Amina Ngahewa

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella ameonya wanaopotosha kuhusu agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwataka wakuu wa mikoa kote nchini kuwatafutia maeneo mbadala wamachinga.

Mongela amesema katika Mkoa Arusha watashirikiana na wafanyabiashara  kuhakikisha wanapata suluhisho  la pamoja katika shughuli ya kuwapatia maeneo mapya.

arushapiccc

Mongella ametoa kauli hiyo leo Jumanne Septemba 14, 2021 baada ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwataka wakuu wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanawapanga wamachinga katika maeneo sahihi.

Soma zaidi: Rais Samia ataka wakuu wa mikoa kuwatafutia maeneo ya biashara wamachinga

"Inawezekana katika kupata suluhisho sio wote watakaoridhika lakini kwa vyovyote vile sisi tutazingatia haki ya kila mtu hakuna atakayeonewa wala kupendelewa kwani tutazingatia haki , taratibu, sheria na maelekezo," amesema

Advertisement

Mongella amewataka wafanyabiashara na wananchi wa mkoa huo kuhakikisha hawajihusishi na matukio ya kuvuruga nia ya kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Naye mwenyekiti wa machinga Mkoa wa Arusha, Amina Njoka amesema  wapo tayari kufuata maelekezo yote watakayopewa na viongozi wao kwa kuwa wanaamini Serikali ina nia njema na wananchi.

Katibu wa wafanyabiashara Mkoa wa Arusha,  Ahmednoor Jamali amesema, “kwa miaka sita tumekuwa tukiteseka wamachinga wamekuwa wakipanga bidhaa zao mbele ya maduka yetu lakini tunaamini wakuu wa mikoa watatekeleza maagizo ya rais na sisi turudi kufanya biashara.”

Advertisement