Agizo la Waziri Jafo lapuuzwa Geita

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo

Muktasari:

  • Agizo lililotolewa mapema Januari 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo kwa halmashauri ya mji wa Geita kuwajengea soko la muda wafanyabiashara wa soko kuu Mbagala halijatekelezwa.

Geita. Agizo lililotolewa mapema Januari 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo kwa halmashauri ya mji wa Geita kuwajengea soko la muda wafanyabiashara wa soko kuu Mbagala halijatekelezwa.

Akiwa kwenye ziara mkoani Geita Januari 5, 2021 Jafo alitembelea soko la Mbagala na kukutana na kilio cha wafanyabiashara wa soko hilo waliolalamikia kukosa wateja kutokana na eneo walilopelekwa kuwa pembezoni mwa mji.

Pia wafanyabiashara hao walilalamikia uwepo wa masoko madogo katikati ya mji pamoja na ubovu wa miundo mbinu ya barabara kuwa ni miongoni mwa sababu zinazosababisha wateja kutokwenda kununua bidhaa kwenye soko la Mbagala.

Kufuatia malalamiko hayo, Jafo alitoa muda wa siku 60 kwa uongozi wa halmashauri ya mji kujenga soko la muda kwenye eneo walilokuwa wakifanya biashara zao zamani kabla ya kuondolewa na halmashauri kutaka kujenga bustani ya watu kupumzika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Nickson Pius amesema soko kuu lilibadilishwa matumizi na kuwa soko la dhahabu na wafanyabiashara kuhamishiwa eneo la Maua ambalo nalo wamehamishwa na kupelekwa soko jipya la Mbagala ambalo liko pembezoni mwa mji.

Wamesema uamuzi wa kuhamia Mbagala umesababisha mitaji yao kufa kutokana na eneo hilo kutokuwa na biashara licha ya kuwa na majengo mazuri yasiyo rafiki kwao kutokana na ubovu wa miundombinu na kukosa mazingira rafiki ya biashara.

Pius amesema uamuzi wa Jafo ulikuwa wa busara lakini hawaelewi nini kimezuia soko hilo kujengwa na kumuomba waziri huyo kuingilia kati.

Wafanyabiashara hao wamesema ikiwa kweli lengo la Serikali ni soko la Mbagala lililogharimu zaidi ya Sh1 bilioni lifanye kazi wanapaswa kuondoa masoko madogo ya Shilabela, Maua na magenge yaliyopo pembezoni mwa barabara ili kuwafanya wateja kwenda kununua bidhaa kwenye soko hilo lililoko pembezoni .

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Geita, Felix Nhalio  amesema suala la soko la muda linasubiri maamuzi ya baraza la madiwani na kwamba wameanza kutekeleza agizo la Waziri na kuwa tayari wamesanifu mchoro wa soko la muda .

Amesema pia wamewasiliana na Tarura kwa ajili ya kujenga barabara zinazozunguka soko la Mbagala na kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi unaendelea.

Soko la mbagala limejengwa kwa fedha zinazotolewa na mgodi wa GGM kwa ajili ya miradi ya jamii(CSR) kwa gharama ya Shilingi bilioni moja.