Ahukumiwa kunyongwa kwa kumuua mkewe apate utajiri

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imemhukumu mkazi wa Kata Mjele, Wilaya ya Mbeya, Mateso Wilson (34) kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua na kunyofoa viungo vya mkewe.

  

Mbeya. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imemhukumu mkazi wa Kata Mjele, Wilaya ya Mbeya, Mateso Wilson (34) kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua na kunyofoa viungo vya mkewe.

Mateso alidaiwa kumuua mkewe Zaina Mela na kunyofoa viungo vyake    yakiwemo maziwa na masikio.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Zawadi Laizer ametoa hukumu leo Jumatano Oktoba 20, 2021 baada ya mahakama kuridhika kuwa ushahidi wa upande wa Jamhuri haukuacha shaka yoyote.

Ilielezwa  mahakamani hapo kuwa mnamo  April  22 , mwaka 2017  mshtakiwa Wilson alishirikiana  kufanya mauaji hayo na wenzake wawili  kwa lengo la kupeleka kwa mganga wa kienyeji ili wapate utajiri wa kudumu.

Wenzake walioshirikiana nao katika mauaji hayo hawajakatwa.

Hakimu Laizer amesema   mahakama imezingatia  maelezo ya pande mbili  na ushauri wazee wa mahakama kabla ya kufikia uamuzi huo.

Mshtakiwa ambaye alikuwa akiwakilishwa na wakili wa kujitegemea, Hilda Mbele    aliiomba mahakama kumpunguzie adhabu.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali,  Davice Msanga aliomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Hakimu Laizer ameeleza mahakama hiyo  kuwa mshtakiwa anahukumiwa kunyogwa hadi kufa  ili iwe fundisho kwa watu wengine ambao wanatafuta mali kinyume cha utaratibu.

Kisheria, ni Mahakama Kuu pekee ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi za mauaji. Hata hivyo Mahakama hiyo inamamlaka ya kutanua wigo wa mamlaka yake na kuziruhusu Mahakama za chini kusikiliza kesi za aina hiyo pale kunapokuwa na mahitaji.