Ahukumiwa miaka 20 jela kwa kusafirisha meno ya tembo

Muktasari:

  • Mahakama ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro imemhukumu kwenda jela miaka 20 Abdallah Salehe (23) mkazi wa Kisiwani kwa kosa la kukamatwa na meno mawili ya tembo wakati akitaka kuyasafirisha.


Same. Mahakama ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro imemhukumu kwenda jela miaka 20 Abdallah Salehe (23) mkazi wa Kisiwani kwa kosa la kukamatwa na meno mawili ya tembo wakati akitaka kuyasafirisha.

Akisoma hukumu hiyo leo Desemba 20, 2021 Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Same, Hellen Hozza amesema mtuhumiwa alifikishwa mahakamani hapo Aprili 22, 2020 akiwa na kesi ya kujibu na kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na jamhuri umethibitisha alimiliki nyara za serikali kinyume cha sheria.

Awali ilielezwa mahakamani hapo na mwanasheria wa jamhuri kutoka hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Samweli Magoko kuwa Machi 27, 2020 mtuhumiwa alikutwa na baiskeli eneo la Kisiwani Wilayani hapo akiwa amefunga mfuko wenye meno hayo ndipo wasamaria wema walipotoa taarifa polisi na mtuhumiwa kukamatwa .

Magoko amesema mtuhumiwa huyo alipohojiwa alikiri kuwa anasafirisha meno kwenda katika eneo la daraja ya Njiro Kisiwani Wilayani Same eneo alilokubaliana kukutana na mteja wake.

Meno hayo mawili yenye uzito wa kg 7.5 yametajwa kuwa na thamani ya Sh33. 6  milioni na yametaifishwa na hakimu Hellen kuwa mali ya serikali.

Imeandikwa na

Dickson Mnzava, Mwananchi