Ahukumiwa miaka 30 kwa kosa la ulawiti
Muktasari:
- Valency Panclas Mtales amehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kwa kosa la kumlawiti kijana mwenye umri wa miaka 24 mkoani Kilimanjaro.
Rombo. Mahakama ya Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro imemhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani, Valency Panclas Mtales(43) mkazi wa kijiji cha Mamsera chini, wilayani humo kwa kosa la kumlawiti kijana mwenye umri wa miaka 24.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Regina Futakamba Machi 22, mwaka huu baada ya mahakama kujiridhisha pasipo na shaka na ushahidi uliotolewa na mashahidi nane wa upande wa mashitaka mahakamani hapo.
Hivyo, Mahakama hiyo chini ya kifungu namba 154 kifungu cha kwanza A cha sheria ya kanuni ya adhabu namba 16 ambayo imefanyiwa marejeo mwaka 2022 ilimtia hatiani mshitakiwa huyo na kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani.
Kesi hiyo namba 196 ya mwaka 2022, ilikuwa na mashahidi nane upande wa mashitaka pamoja na kielelezo kimoja huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi wawili.
Septemba 13, mwaka 2022 majira ya usiku, Mshtakiwa huyo alidaiwa kumwingilia kijana huyo kinyume na maumbile chini ya kifungu namba 154 kifungu cha kwanza A cha sheria ya kanuni ya adhabu namba 16 ambayo imefanyiwa marejeo mwaka 2022.
Kwa sasa mshitakiwa huyo yupo gereza la Ibukoni, wilayani Rombo akitumikia kifungo chake cha miaka 30.