Ajali magari matatu ilivyoua 20

Muktasari:

  • Watu 20 wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu na trekta iliyotokea eneo la Mwakata Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga usiku wa kuamkia juzi.

Kahama. Watu 20 wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu na trekta iliyotokea eneo la Mwakata Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga usiku wa kuamkia jana.

Tukio hilo limetokea zikiwa zimepita siku 13 tangu ajali ya gari iliyoua watu 13, wakiwamo wanafunzi 11 wa Shule ya Msingi ya King David itokee mjini Mtwara.

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Sophia Mjema kufuatia ajali hiyo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Leonard Nyandahu alisema juzi kuwa, chanzo ni uzembe wa madereva wa magari yote matatu aina ya IST, Hiace, lori na trekta lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara.

Kamanda Nyandahu alisema trekta hilo halikuwekwa alama wala kiashiria chochote kuonyesha kuna gari imeegeshwa, hali iliyosababisha Toyota IST kuligonga kwa nyuma kutokana na kutokuwa na viakisi mwanga.

Alisema baada ya ajali hiyo, Toyota Hiace iliyokuwa inatoka mjini Kahama kwenda eneo la Tinde iligongana uso kwa uso na lori wakati akitaka kuikwepa IST baada ya kuigonga trekta katika ajali ya kwanza.

“Uchunguzi wa awali umebaini hata madereva wa Toyota Hiace na Fuso (lori) nao hawakuchukua tahadhari wakati wanapita eneo la ajali ya awali, ndiyo maana waligongana uso kwa uso,” alisema Kamanda Nyandahu.

Hata hivyo, aliwataka madereva kuendesha kwa tahadhari na kutii sheria za usalama barabarani.

Kilevi chakutwa ndani ya gari

Akizungumzia ajali hiyo, Mjema alisema askari polisi walikuta chupa kubwa ya pombe kali aina ya K-Vant ikiwa nusu ndani ya moja ya magari yaliyohusika kwenye ajali, hali inayoonyesha waliokuwamo ndani ya gari hilo walikuwa wanakunywa wakiwa safarini au walikuwa wamekunywa kabla ya kuanza safari.


Matukio ya ajali

Matukio mawili ya ajali ya Mtwara iliyoua watu 13 na Kahama yaliyosababisha vifo vya watu 20, yanafanya idadi ya watu waliopoteza maisha na ajali nyingine za barabarani Juni 10 hadi Julai 13 kufikia 83.

Matukio mengine ya ajali yaliyoripotiwa sehemu tofauti nchini ni lile la Juni 30 lililohusisha gari aina ya Toyota Wish iliyotokea eneo la Luguru Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, watu watano walifariki dunia huku wengine watano wakijeruhiwa.

Julai 12 eneo la Magereza, nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu, watu watano walifariki dunia na wengine 11 wakijeruhiwa baada ya magari madogo mawili aina ya Toyota Pro Box na Toyota Wish kugongana.

Akizungumzia matukio ya ajali yanayoripotiwa sehemu mbalimbali nchini, Katibu wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Hashim Omari alitaja ukaidi wa sheria za usalama barabarani, uzembe wa madereva na watumiaji wengine wa barabara kuwa chanzo cha ajali zinazoangamiza maisha ya watu wasio na hatia.

“Tunatoa matamko kila siku lakini kila kukicha tunashuhudia ajali ambazo nyingine zinatokana na uzembe wa madereva kama hii ya Kahama, dereva wa trekta aliliegesha bila kuweka ishara yoyote ya tahadhari na kusababisha ajali ya magari mengine matatu na kuua watu 20,” alisema Omari.

“Nadhani imefika wakati tuache matamko ya kisiasa kuhusu usimamizi wa sheria za usalama barabarani, kwa mfano tungekuwa na askari wa doria wa kutosha katika barabara kuu ya Kahama – Shinyanga, pengine lile trekta lingeonekana mapema na kuondolewa barabarani.”

Mdau huyo wa usalama barabarani aliwasihi askari wa usalama barabarani kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwachukulia hatua wote wanaokiuka sheria bila kujali hali zao kiuchumi wala nafasi zao.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbrod Mutafungwa alitembelea eneo la ajali hiyo jana na kuwataka madereva nchini kufuata sheria za usalama barabarani na kuwa makini.


Mashuhuda

Mabula Chande, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo ya jana ameunga mkono kauli ya Jeshi la Polisi kuwa uzembe wa madereva ndiyo chanzo cha ajali.

“Pamoja na kukosa umakini, madereva wa hiace na lori pia walikuwa wakiendesha kwa mwendo kasi ndio maana walishindwa kufunga breki walipofika kwenye eneo la ajali ya IST na trekta. Wangekuwa kwenye mwendo wa kawaida wangefunga breki na kusimama,” alisema Chande.

Kauli kama hiyo pia ilitolewa na John Maduhu, akisema, “kwa idadi ya vifo na majeruhi katika ajali hii, hasa ile iliyohusisha Toyota Hiace na lori ni wazi magari yote mawili yalikuwa kwenye mwendo kasi na madereva wakashindwa kufunga breki.”

Maduhu aliwaomba madereva wanapopita eneo lilikotokea ajali kuchukua tahadhari si tu ya ajali zinazohusisha magari, bali pia mikokoteni inayokokotwa kwa punda, hasa nyakati za usiku kwa sababu nyingi hazina alama wala viakisi mwanga.


Majeruhi wapewa rufaa

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Deogratius Nyaga alisema miili ya watu 20 na majeruhi 15 ilipokewa huku majeruhiwa watatu wakiwa katika hali mbaya.

Alisema majeruhi hao walitarajiwa kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga au Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kwa uchunguzi na matibabu zaidi ya kibingwa.