Ajali za majini zinavyoangamiza maisha ya watu Ziwa Victoria

Ajali za majini zinavyoangamiza maisha ya watu Ziwa Victoria

“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” Huo mmoja wa mistari iliyomo katika mafundisho ya Biblia katika kitabu cha Hosea 4:6.

Usemi huo ndiyo unaweza kutumika kuzungumzia ajali za majini ndani ya Ziwa Victoria, sababu zake na idadi ya watu wanaopoteza maisha kutokana na ajali hizo.

Takwimu kutoka Shirika la Uwakala wa Meli nchini (Tasac) zinaonyesha kuwa watu 363 walifariki dunia kutokana na ajali 43 zilizotokea ndani ya ziwa hilo kati ya Februari 19, 2009 hadi Juni 23, 2020.

Jumla ya watu 884 walihusika kwenye ajali hizo zilizotokea katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera na Geita ambapo watu 521 waliokolewa.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Emmanuel Ndomba anasema idadi ya vifo vinavyotokana na ajali ndani ya Ziwa Victoria ni kubwa kulinganisha na taarifa rasmi zinazoripotiwa kwa sababu taarifa nyingi za ajali haziripotiwi kwenye mamlaka husika.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, inakadiriwa kuwa watu wawili hufariki dunia kila siku kutokana na ajali za majini ndani ya Ziwa Victoria.


Sababu za ajali

Ofisa Mfawidhi wa Tasac Mkoa wa Geita, Rashid Katonga anataja uzembe wa kibinadamu, vyombo vya usafirishaji kukosa ubora unaostahili, manahodha kukosa ujuzi na weledi pamoja na wasafiri kutovaa jaketi okozi (maboya) wakati wa safari kuwa ni baadhi ya sababu zinazosababisha ajali za majini na watu wengi kupoteza maisha.

“Kisheria, vyombo vyote vya majini vinatakiwa visajiliwe baada ya kukaguliwa uimara, ubora, ujuzi na weledi wa manahodha pamoja na vifaa vya uokoaji kabla ya kuingia majini. Lakini wamiliki wengi hukiuka sheria hii na matokeo yake ni ajali ambazo zingeweza kuzuilika,” alisema Katonga.


Mikakati kudhibiti ajali

Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya usafirisaji majini imeanza kutekeleza mikakati kadhaa ikiwemo ujenzi wa vituo 10 vya ufuatiliajali na uokoaji na kudhibiti ajali zinazotokea ndani ya Ziwa Victoria.

Mradi huo utakaogharimu zaidi ya Sh4.2 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), utahusisha ujenzi wa kituo kikuu cha kuratibu shughuli za ufuatiliaji na uokoaji ndani ya ziwa hilo pembezoni mwa Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Wakati kituo hicho kikijengwa wilayani Ilemela, vituo vingine vitajengwa eneo la Bandari ya Mwanza Kusini jijini Mwanza, Darajani-Chato, Musoma, Mwibara, Nansio-Ukerewe, Kakukuru-Ukerewe, Magarini-Muleba, Kemondo na Ukara-Ukerewe.

Vituo hivyo ambavyo sita tayari mchakato wake ikiwemo michoro umekamilika vitajengwa katika mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na Kagera.

“Pamoja na Tanzania inayomiliki asilimia 51 ya Ziwa Victoria, miradi ya ujenzi wa vituo vya ufuatiliaji na uokoaji pia inatekelezwa katika nchi za Uganda na Kenya kwa lengo la kuongeza uwezo wa kukabiliana na kudhibiti ajali na majanga ndani ya Ziwa Victoria,” alisema Ndomba.

Kaimu Msajili wa Meli, Alfred Wariana aliwaambia waandishi wa habari jijini Mwanza kuwa taarifa zote za ajali na majanga zitapokewa katika kituo kikuu cha kuratibu shughuli za ufuatiliaji na uokoaji wilayani Ilemela kitakachokuwa na vyombo vya kisasa vya mawasiliano.

“Baada ya kupokelewa, taarifa hizo zitarushwa kwenye vituo vingine vya ufuatiliaji na uokoaji kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za uokoaji,” alisema Wariana.

Pamoja na vifaa vya uokoaji majini, alisema vituo hivyo pia vitakuwa na magari ya zimamoto na vifaa vingine vya mawasiliano.

Sheria kuminya zaidi

Pamoja na elimu kwa umma kuhusu kanuni za usalama, Serikali pia inakusudia kuongeza makali ya sheria, kanuni na taratibu za ubora na usalama katika vyombo vya usafirishaji majini kudhibiti vifo vinavyotokana na ajali na majanga majini.

Akizungumza na wadau wa usafirishaji majini katika mialo ya mkoa wa Geita jana, Ndomba alisema pamoja na kuhakikisha vyombo vyote vya usafirishaji majini vinakuwa na vifaa vya uokoaji ikiwemo jaketi okozi (maboya) kulingana na idadi ya abiria, sheria hiyo itakayotoa faini na kifungo jela pia itawawajibisha abiria wasiovaa maboya wakati wa safari.

“Kila anayesafiri majini atalazimika kuvaa maboya kama ilivyo lazima abiria wanaosafiri kwa njia ya barabara na angani kufunga mikanda,” alisema Ndomba wakati akizungumza na wadau katika mialo ya Nkome, Ujaluoni, Makatani na Runazi wilayani Geita

Kwa sasa, sheria inawabana wamiliki kuhakikisha vyombo vyao vinakuwa na maboya kulingana na idadi ya abiria; lakini hakuna sheria inayowabana abiria wanaokaidi kuvaa maboya.

“Nia ya Serikali ni kuona hakuna anayepoteza maisha hata pale ajali zinapotokea majini. Na njia ya kufikia lengo hilo ni wamiliki wa vyombo, wafanyakazi na abiria wote kuzingatia kanuni za usalama kabla ya kuanza na wakiwa safarini,” alisema Ndomba.

Pamoja na udhibiti na kusimamia huduma za bandari, Tasac pia ina jukumu la kusimamia ulinzi, usalama wa vyombo vya usafiri majini, utunzaji wa mazingira na kusimamia shughuli za biashara ya meli.

Akizungumzia vifo vinavyotokana na ajali za majini, mmoja wa abiria aliyekutwa katika mwalo wa Ujaluoni, Bundala Lubinzagula alishauri itungwe sheria inayolazimisha si tu uvaaji wa maboya, bali pia wamiliki kukata bima kwa abiria na vyombo vya usafirishaji majini.

“Kama ilivyo kwa magari, vyombo vya usafirishaji majini pia viwe na bima ya ajali kuwezesha waathirika kulipwa fidia,” alisema Lubinzagula.

Scolastica Malongo, mmoja wa abiria aliyekuwepo mwalo la Nkome aliiomba Serikali kuhakikisha maboya ya watoto pia yanakuwepo katika vyombo vya usafirishaji majini huku akihoji kwanini abiria katika vivuko vya Serikali na watu binafsi hawavai maboya.

Historia ya ajali Ziwa Victoria

Miongoni mwa ajali za majini ndani ya Ziwa Victoria zilizowahi kutikisa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla ni ile ya meli ya Mv Bukoba na kivuko cha Mv Nyerere.

Ajali ya Mv Bukoba ilitokea Mei 21, 1996 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 baada ya meli hiyo kupinduka na kuzama ikiwa kilomita chache kufika bandari ya Mwanza.

Septemba 20, 2018, Taifa lilikumbwa na ajali nyingine kubwa baada ya kivuko cha Mv Nyerere kupinduka na kuzama hatua chache kabla ya kutia nanga bandari ya Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe ambapo watu 227 walipoteza maisha.

Imeandikwa na Peter Saramba