Ajeruhiwa na simba akiokoa mifugo

Muktasari:

  • Mkazi wa kitongoji cha Songambele kijiji cha Nyichoka wilayani Serengeti, Mgusui Chacha(32) amejeruhiwa na simba wakati akitoka kuchunga mifugo.

Serengeti. Mkazi wa kitongoji cha Songambele kijiji cha Nyichoka wilayani Serengeti, Mgusui Chacha(32) amejeruhiwa na simba wakati akitoka kuchunga mifugo.

Akizungumza leo Alhamisi Januari 14, 2021 mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema mwananchi huyo alijeruhiwa na simba jana na amelazwa hospitali ya Nyerere.

“Alivamiwa wakati anajaribu kuokoa mifugo ili isivamiwe na wanyama hao, Simba mmoja alikuwa amebana pembeni ndiye aliyemvamia na kumjeruhi mkono wa kushoto na aliokolewa na wananchi, matukio ya simba kula mifugo kwenye vijiji hayo yanaripotiwa mara kwa mara, " amesema.

Ofisa wanyamapori Wilaya ya Serengeti, John Lendoyan amesema SImba wanajificha milimani na jioni huonekana vijijini na kwamba wanaandaa utaratibu shirikishi wa taasisi nyingine ili kuwadhibiti.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Nyichoka,  Peter Kairo ameiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwa mifugo inazidi kuliwa na wanyamapori hao.

“Wanatakiwa kuwahamisha hawa wanyama kama ilivyofanyika mwaka jana, waliwaondoa simba 36  na kuwapeleka Burigi Chato..., kwa kweli tulipumua ila sasa wameibuka tena ni hatari kwa watu na mifugo," amesema.