Ajinyonga baada ya kukataliwa na mpenzi wake

Ajinyonga baada ya kukataliwa na mpenzi wake

Muktasari:

  • Kaka wa marehemu amesema siku moja kabla ya kifo cha ndugu yao, mpenzi wake alifika nyumbani kwao na kusema kuwa hamtaki.

Serengeti. Kitachana Shenani (30) mkazi wa kitongoji cha Senta kijiji cha Makundusi Wilaya ya Serengeti amejijyonga kwa kamba hadi kufa baada ya kukataliwa na mpenzi wake.


Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti Cosmas Qamara kwa niaba ya Mkuu wa wilaya Nurdin Babu leo Jumatatu Aprili 12 amesema tukio hilo limetokea aprili 11 majira ya saa 11 jioni.


Amesema, Shenani alikataliwa na mpenzi wake Pilly Kikono (39) mfanyabiashara ya viatu kijiji cha Natta mbele ya familia kwa madai kuwa amekuwa akimfanyia fujo ikiwemo kumpiga.


Kaka wa marehemu Jokonasi Shenani ameliambia Mwananchi kuwa Aprili 11 mpenzi wake huyo alimkataa mbele yao kuwa hamtaki atafute mwanamke mwingine.


"Alikuja na nguo zake akatukabidhi na kudai kuwa hataki kumuona tena kwake lakini mdogo wangu akadai hakubaliani na uamzi huo kwa kuwa anampenda sana na huenda amepata mwingine," amesema.


Amesema jioni alipata taarifa ya kujinyonga kwake kupitia wachunga mifugo
"Inashangaza sana kwa kuwa familia ilimtaka atafute mke aoe," amesema.


Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Makundusi Mseti Nyaikobe amesema, baada ya uchunguzi wa polisi na mganga na kubaini chanzo cha kifo ni kujinyonga familia imekabidhiwa mwili na taratibu za maziko zinaendelea.