Ajira za muda kada ya afya zaja

Wednesday September 15 2021
ajira kada za afya pic
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Wakati wataalamu mbalimbali kada ya afya wakikabiliwa na ufinyu wa ajira, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekamilisha mwongozo wa kitaifa kwa ajili yakuwawezesha wahitimu kuajiriwa.

Mwongozo wa kitaifa wa kujitolea (National Health Workforce Volunteerism Guideline) unaotoa utaratibu wa namna bora ya hospitali na vituo vya afya kutumia wahitimu wa kada ya afya ambao hawajaajiriwa ili waweze kutumika rasmi katika utoaji wa huduma za afya kwa njia ya kujitolea.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 15, 2021 na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima wakati akifungua mkutano mkuu wa waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri mjini Dodoma.

“Mwongozo huo ni mkakati mahususi wa kuboresha huduma za afya kwa kukabiliana na uhaba wa watumishi katika sekta ya afya nchini hii hapa ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa upatikanaji na utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi,” amesema.

Waziri Gwajima, amesema Serikali ya awamu ya sita inaendelea kutekeleza afua za sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi 2,726 wa kada za afya kwenye mamlaka za serikali za mitaa, lengo likiwa kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.

Advertisement