Akutwa amekufa pembeni kukiwa na ujumbe ‘mke wa mtu ni sumu’

Akutwa amekufa pembeni kukiwa na ujumbe ‘mke wa mtu ni sumu’

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro  amesema watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya mtu mmoja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40-42 yaliyotokea katika mtaa wa Kanyerere kata ya Mkuyuni mkoani humo.

Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro  amesema watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya mtu mmoja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40-42 yaliyotokea katika mtaa wa Kanyerere kata ya Mkuyuni mkoani humo.

"Kando ya mwili wa marehemu kulikutwa ujumbe uliosomeka kuwa 'mke wa mtu ni sumu' watuhumiwa wanahojiwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani," amesema Muliro jana Jumatano Machi 31, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Wakati huohuo, amesema wanamshikilia Mengi Muheta ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi  Kishiri pamoja na wenzake 18 kwa tuhuma za wizi wa vitabu 529 vya shule za msingi.

Watuhumiwa hao wamekamatwa katika msako ulioendeshwa kati ya mwezi Februari na Machi, 2021 na kwamba vitabu hivyo ni vya shule ya msingi Bujingwa, Igoma na Manguluma zote za wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Muliro amesema vitabu hivyo viliibwa kwa nyakati tofauti baada ya watuhumiwa kuvunja ofisi za shule hizo.

"Uhalifu huo umefanywa na walimu, walinzi na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wanataka kuvinunua jijini Mwanza ambapo ili kuidhinisha uhalifu huo walikuwa wanafuta alama maalumu inayowekwa kuashiria vinamilikiwa na serikali inayosomeka "hakiuzwi" ili waweze kuviuza kwa urahisi."

"Baada ya kuwakamata tunaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika wote, upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani,” amesema.

Pia, wanawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kusafirisha gunia sita zilizokuwa na dawa za kulevya aina ya bangi katika kata ya Buswelu wilaya ya Ilemela.