Ali Kiba anapomwimbia mapenzi mwanaume

Ali Kiba anapomwimbia mapenzi mwanaume

Muktasari:

“Sikatai yule mwonyesha wivu ndiye mwenye mapenzi ya kweli kwa mwenzi.

“Vesi No 1”

“Sikatai yule mwonyesha wivu ndiye mwenye mapenzi ya kweli kwa mwenzi.

Lakini pia uvumilivu na vitendo vya karaha vilimuumiza. Mwenzio mimi ni mtulivu na kuiba mali ya mtu sijafunzwa.

Ona dhambi lawama ulonipa mimi leo inaniuma eh. Fikira zako ziko vibaya kwa kudhani ya kwamba yule demu nilimpenda. Ni kweli nilimpendaaa, lakini ni kama rafiki wa Kiba. Haya ulofanya leo, ikifika kesho utajibu nini kiama. Kwa yale yote mapendo ni kama kioo aliyokupa niliyaona. Ukadhani anakusaliti kutoka kwako na kuwa mimi naye. Mimi na yeye. Kutokana na wako wivu ukadiriki kumuacha ajiue. Kwa nini, unatema Big G kwa karanga za kuonjeshwa. Najua mwanamke akipenda, huwaa... kapenda kweli.”

(Mapenzi yana-run dunia, mapenzi yana-run dunia) x6.

Wengi wakiusikia huu wimbo hudhani mshikaji anaiimbia pisi flan hivi. Ama pisi zote kiujumla. Ukweli Kiba anamuimbia mapenzi msela tu. Wengi husikiliza na kukariri. Lakini hatuzingatii kujua mwana alimaanisha nini. Unahitaji sikio la tatu kumuelewa Kiba, kwenye wimbo huu wa “Mapenzi Yanarun Dunia”. Na hapa ndipo anapojitofautisha Kiba na wenzake.

Bonge moja na ngoma. Na kila mtu ukimfafanulia alicholenga King Kiba, huduwaa. Kujua anaimbiwa mshikaji tu wengi hawajui. Wanaishia kusikiliza sauti tamu, maneno mazuri ya mapenzi na mdundo husika. Zaidi ya hapo hawaelewi mlengwa wa mashairi hayo. Katika hili huenda hata shemeji Amina, pale Mombasa, hajang’amua.


“Vesi No 2”

“Wajua kuna waliobadilisha dini na yote sababu ya kupenda. Na kuna walokimbia, hii dunia, sababu hiyo hiyo kupenda. Yule alikupenda sana, ninajua na mambo mengi umefanya. Ila best wangu nilimpenda, umefanya mpaka sasa kajiua. Fikira zako ziko vibaya kwa kudhani ya kwamba yule demu nilimpenda. Ni kweli nilimpendaaaa lakini ni kama rafiki wa Kiba. Haya ulofanya leo, ikifika kesho utajibu nini kiama. Kwa yale yote mapendo ni kama kioo aliyokupa niliyaona. Ukadhani anakusaliti kutoka kwako na kuwa mimi naye. Mimi na yeye

Kutokana na wako wivu ukadariki kumuacha ajiue. Kwa nini (why). Unatema Big G, kwa karanga za kuonjeshwa. Najua mwanamke akipenda, huwaa, kapenda kweli.”

(Mapenzi yana-run dunia, mapenzi yana-run dunia) x6.


Kuna wakati watu waliamini kwamba wanamuziki wa kuimba wanatunga vitu vyepesi na hawawezi kuzama ‘dipu’ katika fikra zao na kuibuka na kitu ambacho ama kitashangaza au kuleta mtihani wa kuelewa.

Lakini King Kiba, alikata daraja la fikra hizo. Wimbo kama huu ni Hip Hop katika mashairi na mtindo wa kuimba. Yes! Wapo kina Nate Dog (RIP) walikuwa namna hii.

Kiba kacheza na maneno ambayo bila kuweka ufundi wake wengi wangepata taabu kuelewa anaimba nini.

Kifupi ni kwamba aliimba kitu kigumu chenye kustahili huzuni na hasira dhidi ya muhusika, lakini sauti, maneno na namna alivyowasilisha kafanya kionekane kitu kitamu cha kulilia penzi.

Labda tuwekane sawa. Kiba ameimba kuhusu mshikaji ambaye alimuacha mpenzi wake ajiue. Kwa hisia zake za kidwanzi kuwa anatoka na Kiba. Kumbe pisi ilikuwa inamuelewa sana mpenzi wake huyo. Kiba alikuwa rafiki wake tu hakukuwa na lolote la mapenzi. Pisi ilipotemwa ikabembeleza penzi lake bila mafanikio.

Pisi ikaona kwamba kuna sababu gani ya kuishi bila penzi la jamaa yake. Kuna haja gani ya kuwepo duniani huku yule mwanaume ampendaye hataki tena. Na sababu ni kuhisi anatoka na Kiba, kitu ambacho siyo kweli. Pisi ikaamua kujiua. Na jamaa akaridhia kabisa ijiue kiroho safi. Maumivu.

Haya mambo yapo sana mitaani. Kuna ndoa na uhusiano huvurugika kwa hisia tu. Mtu anaona dem wake yupo karibu na msela flani, anajua mali yake yaliwa. Wengi wetu hatuna uvumilivu, tunavuta bangi badala ya subira. Tunawatema wanaotupenda kwa hisia tu. Tubadilike sasa kupitia ngoma hii ya King Kiba.

Lakini pia pisi zijue mazingira ya kuishi na marafiki zao wa kiume. Weka mipaka ambayo haiwezi kuleta hisia mbaya kama mnatoka au lah. Siyo urafiki wa kuvuka mipaka kiasi cha kushikana hata nyonga mnapopita mitaani. Na hiyo iwe kwa masela pia, tofautisheni rafiki na pisi yako namna ya kuishi.

Mnaitana wenyewe baby sijui mara darling na Shem darling. Tuliotoka kule Tarime hizo swaga tunapita na shingo hiyo. Hatuwezi kukuelewa na tutaona unaleta mapicha picha tu. Tutakupiga tu. Na mimi nasema mpigwe tu. Eeeeh, maana hamna namna. Mnaambiwa muishi kishikaji nyie mnaleta ulaazizi? Mpigwe tu.

Ngoma za namna hii zilikosa kitu kimoja tu. Video kali! Zilitoka wakati ambao bado tupo nyuma kiaina katika teknolojia ya video za muziki. Mating’a kama yale yangekutana na ‘fulu echidii’. Pisi kali za video vixen. Promo la insta na fujo za Twitter na Facebook! Amini nakuambia Bongo ingesimama.

Teknolojia ya video haikuwa mbaya sana, hasa ukitazama kazi za wengine zilizotoka wakati huo. Ukweli ni kwamba King Kiba mwenyewe, hakuwahi kuwa na mzuka wa video kali. Amekuja kubadilika wakati huu wa ushindani wa Mondi na kimataifa zaidi. Kaanza kuweka kitu juu ya kitu.

Hapo kabla mtoto wa Kimanyema aliamini katika uwezo wake wa sauti, kutunga ngoma kali na mapenzi mazito toka kwa mashabiki hasa wa kike, ambao walifunga ndoa na ngoma za kijana huyo wa Kariakoo.

Kuna totozi akitoa ngoma yoyote wao hupokea kibabe mno, huwaambii kitu na hawana muda wa kujiuliza kama kali au lah.

Ndio faida ya kutengeneza jina mapema. Mtu kama Kiba, alifanya kazi mwanzoni wakati anatoka. Hii leo inakuwa rahisi kwa sababu tayari alishawaaminisha watu kuwa ni nani. Tengeneza msingi wako vizuri ili mbeleni uamue kuezeka kwa bati, kigae au zege tu. Msingi si upo imara.

Undava na unyama aliofanya katika ngoma kama hizi ndiyo sababu ya yeye kuvimba leo. Kazi ya sasa inayofanywa na Harmonize, kuaminisha anaweza mbele ya kina Ben Pol, Barnaba na wengineo, Kiba alifanya miaka 13 nyuma mbele ya wakali kama TID, Chillah, Ruta Bushoke na Banana Zorro.

Leo hii Ali Kiba anaenjoy maisha ya muziki, kitu hiki kinawashinda wengi wao kwa sababu wanashindwa kuenjoy muziki. Kiba hapanii, anachofanya ni kile anachoamini kutoka ndani yake. Wale wengine huwaza nyumba, ndinga na totozi za Mondi badala ya muziki.

Ndio maana unaona Kiba, anabaki kuwa mshindani mkubwa wa Diamond. Ogopa mtu anayefanya muziki akitabasamu. Humfanya ageuke lulu katikati ya tope zito. Marehemu Mohammed Ali, aliwaua wenzake kwa tabasamu lake ulingoni. Anakupiga huku anacheka.

Tuwe wakweli wanamuziki wa zamani wanashindwa kufikia alipo Kiba. Kwa sababu ya kupania na kukosa utulivu, mtu unaingiza sauti huku unawaza clip ya Diamond akimpokea Koffi Olomide! Lazima uchemke. Muziki unahitaji mtu anayefurahia maisha.

Unaimbia watu ili wafurahi. Mwimbaji mwenyewe umekunja sura ka’ jongoo aliyepigwa teke. Muziki ni furaha hata kama unaomboleza. Hivi sasa Kiba chochote atakachotoa kinapokelewa. Kazi ya kuaminisha watu aliimaliza kitambo sana.