Alichokisema mke wa mtendaji aliyeuawa Dar

Muktasari:

  • Ikiwa ni siku moja imepita tangu kuuawa kwa Kelvin Mowo ambaye alikuwa mtendaji wa kata ya Msumi akiwa ndani ya ofisi yake, mke wake Marietha Richard amefunguka mazito.

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku moja imepita tangu kuuawa kwa Kelvin Mowo ambaye alikuwa mtendaji wa kata ya Msumi akiwa ndani ya ofisi yake, mke wake Marietha Richard amefunguka mazito.

Kupitia ukurasa wake wa Facebok, ameandika ujumbe uliojaa machungu na kuonyesha jinsi gani kuondoka kwake kumemuachia simanzi kubwa.

“Bora ungeumwa nikakuuguza, umeniacha mjane kweli Kelvin wangu? Mtoto wetu nitamwambiaje? Kweli leo unaitwa marehemu Kelvin Costa Mowo? Hapana, mbona bado mapema?” ameandika Marietha.

Marietha ambaye pia ni mjamzito, ameonyesha masikitiko yake huku akisema mume wake hakutaka kusubiri ili amuone mtoto wao atakapozaliwa na kumpa jina zuri.

“Mume wangu ulieniheshimisha, rafiki yangu kipenzi tuliishi kama watoto vile. Amka baba yangu Kelvin unaniaga asubuhi unaenda kazini nifiche mtoto asikutazame ukitoka kumbe hukutaka kumuaga mtoto wako?” ameandika mwanamke huyo.

Ameandika kuwa hadi siku ya tukio jana saa saba mchana, alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi wa orodha ya  vitu vya kununua wakati anarudi kutoka kazini bila kujua kwamba tayari ameuawa.

"Mume wangu mcheshi, mkarimu, Yesu mpokee mtumishi wako. Kelvin wangu ulinipenda kwa dhati ndio maana ukanioa mimi Marietha Richard wako. Kelvin naandika nikiamini utasoma mpenzi wangu, maana tunaonaga kwenye movie na uliniambia siku ukifa utasoma nitakachokiandika.

Wakati akiandika ujumbe huo, amedai kuwa alikuwa akitetemeka, akiandika na kufuta huku akijiuliza kama ni kweli mumewe anasoma.

“Natamani nisikie ukinijibu ndio unasoma. Kelvin mume wangu nakupenda sana. Natamani lile kumbatio lako la jana nje getini nilipokupokea ulipotoka kazini nilipate tena wakati huu. Ooh jamaani walimwengu mmekatisha uhai wa kijana mdogo, mchapa kazi. Yesu asante mpokee tu,” ameandika Marietha.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumuua Kelvini.

Aliuawa Jumatatu Oktoba 11, 2021 saa 5 asubuhi alipokuwa akisikiliza mgogoro wa ardhi.