Alicia Keys ‘awatuliza’ mashabiki wa Diamond

Saturday December 19 2020
aliciakeyspic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Unaweza kusema kiu ya mashabiki wa msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz imetulia.

Hiyo ni baada ya msanii wa Marekani, Alicia Keys kutoa remix ya wimbo Wasted Energy huku Diamond akiimba muda mrefu zaidi tofauti na wimbo wa kwanza ambao msanii huyo aliimba takribani sekunde 25 na kuibua maneno kwenye mitandao ya kijamii.

Wimbo huo uliotoka leo Ijumaa Desemba 18, 2020 mbali na Diamond kuimba zaidi, Alicia Keys amemshirikisha msanii mwingine wa Marekani, Kaash Paige.

Dakika chache baada ya kuachia wimbo huo Alicia aliweka video mtandaoni akionekana akiwa studio akisikiliza wimbo huo na kuambatanisha maneno, “mliomba wimbo huu! Hakika mapenzi yenu juu ya Wasted Energy ni ya moto sana. Na sasa Diamond na Kaasha Paige wamefanya mambo makubwa humu ndani.”

Wimbo huo mara ya kwanza ulitoka Septemba, 2020 na Diamond aliimba sekunde hizo wakati wimbo huo ni wa dakika nne na sekunde 19.

Jambo hilo liliibua mjadala mitandaoni huku mashabiki wa Diamond wakivamia  kurasa za mitandao ya kijamii ya Alicia na kulalamikia suala hilo.

Advertisement

Hali hiyo ilimuibua mume wa msanii huyo wa Marekani, Swizz Beatz  ambaye alimuomba Diamond kuwatuliza mashabiki wake kwa kuwaeleza ukweli kuwa ni yeye ndio  aliyechagua kuimba kipande kidogo si kama alipangiwa kufanya hivyo

Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, Diamond aliweka wazi kwamba kuna kazi nyingine nyingi amefanya na Alicia Keys na zitatoka hivi karibuni.


Advertisement