Alikiba aimba na kucheza wimbo wa Diamond, Zuchu na Harmonize

New Content Item (2)
Alikiba aimba na kucheza wimbo wa Diamond, Zuchu na Harmonize

Muktasari:

  • Alikiba, mkali wa muziki wa Bongofleva anayetamba na wimbo wa Infidele  amejirekodi video akicheza na kuimba baadhi ya nyimbo za wasanii wenzake wa Tanzania, akiwemo Diamond Platnumz, Harmonize na Zuchu.


Dar es Salaam. Alikiba, mkali wa muziki wa Bongofleva anayetamba na wimbo wa Infidele  amejirekodi video akicheza na kuimba baadhi ya nyimbo za wasanii wenzake wa Tanzania, akiwemo Diamond Platnumz, Harmonize na Zuchu.

Uamuzi wake huo umeibua mjadala mtandaoni hasa kutokana na ushindani wa muziki kati yake na Diamond ambaye ni bosi wa lebo ya Wasafi yenye wasanii wengine akiwemo Zuchu, Lavalava, Rayvanny, Mbosso na Queen Darlin .

Jana Ijumaa Februari 26, 2021, Alikiba  ndio aliweka video hizo katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Akionekana kuwa katika chumba ambacho shughuli ya mapishi ilikuwa ikiendelea, msanii huyo alikuwa akisikiliza nyimbo za wasanii mbalimbali na kueleza jinsi zilivyo nzuri kwenye utunzi, uimbaji  na video.

Wimbo wa Diamond aliousikiliza ni  African Beauty ambao msanii huyo alimshirikisha msanii wa Marekani, Omarion na Alikiba aliimba ubeti wa pili wa  wimbo huo ulioimbwa na Omarion.

Wakati ukisikika wimbo wa Sukari wa Zuchu, msanii huyo alionekana akiimba na kucheza PAMOJA NA WIMBO WA Happy birthday wa Harmonize.

Alikiba yupo Afrika Magharibi kwa ajili ya kukutana na wasanii mbalimbali atakaowashirikisha katika album yake atakayoitoa mwaka 2021.