Aliyedaiwa kumtoboa jicho mkewe kisa mjomba akamatwa

Jackline Mnkonyi ambaye amefanyiwa ukatili na mumewe kumng'oa jino la kumtoboa jicho.

Muktasari:

  • Siku chache baada ya kufanya tukio la ukatili kwa kupiga, kumng’oa jino kwa plaizi na kumtoboa jicho mkewe kwa bisibisi, mtuhumiwa Isack Robertson amekamatwa jana akiwa Himo mkoani Kilimanjaro.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha katika maeneo ya Himo mkoani Kilimanjaro limefanikiwa kumkamata Isack Robertson (45) mkazi wa Sombetini jijini Arusha kwa tuhuma za kumtoboa jicho na kumng’oa jino mkewe Jackline Mkonyi (38) mkazi wa Sombetini jijini Arusha kwa kile kinachodaiwa wivu wa mapenzi.

Hayo yamesemwa leo Mei 28, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo kupitia taarifa maalum kwa umma iliyoeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa jana Mei 27.

Amesema mpaka sasa mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapalekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linatoa onyo kwa baadhi ya watu wachache wanaofanya vitendo vya ukatili katika familia zao ama sehemu nyingine kuacha mara moja, kwani kwa kuendelea kufanya vitendo hivyo hatutasita kuwakamata.

“Pia niwaombe wananchi popote walipo wasifumbe macho vitendo viovu na waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao ili kukomesha matukio hayo,” amesema ACP Masejo.

Mtuhumiwa huyo alimfanyia ukatili huo mkewe Mei 23 saa nne usiku kutokana na wivu wa mapenzi baada ya kumpokea mjomba wake nyumbani kwake mchana.

Mjomba wa mwanamke huyo, ambaye ni Vicenti Matai baada ya kuondoka mumewe alifika nyumbani na kuanza kumuhoji juu ya mgeni huyo na baadaye kumfanyia ukatili huo.

Baada ya kumng'oa jino na kumtoboa jicho, alimpeleka kwa wazazi wake eneo la Daraja Mbili jijini Arusha na kumtelekeza nje ya nyumba usiku na kutoweka.