Aliyekuwa diwani Chadema, wenzake waachiwa huru

Watu saba wafikishwa kortini wakidaiwa kujipatia Sh 428milioni mali ya Tanesco

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imemuachia huru aliyekuwa Diwani wa Isengule wilayani Tanganyika (Chadema), Oscar George na wenzake watano, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuwasilisha vielelezo katika kesi ya mauaji iliyokuwa inawakabili.

Katavi. Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imemuachia huru aliyekuwa Diwani wa Isengule wilayani Tanganyika (Chadema), Oscar George na wenzake watano, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuwasilisha vielelezo katika kesi ya mauaji iliyokuwa inawakabili.

Maamuzi hayo yalifikiwa juzi Alhamisi, Agosti 4, 2022 na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Dunstan Ndunguru kutokana na shauri hilo kuendeshwa kwa njia ya mtandao na kuamuru watuhumiwa kuachiwa huru, baada ya kukaa rumande zaidi ya miaka mitatu tangu 2019.

Wafuasi wengine wa Chadema walioachiwa huru na mahakama hiyo ni Lespice Elias, Emmanuel Mzerani, Busiga Clement, January Kahutu na Mickson Makatare.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela amesema wanaishukru mahakama kwa uamuzi huo akidai kuwa walikamatwa kwa chuki za kisiasa.

“Hiyo kesi ilikuwa ya mchongo lakini tunashukru sana, hii imetokana na na maridhiano yanayoendelea baina ya chama na Serikali japo wanachama wetu wameathirika sana mfano diwani alikatizwa kuwatumikia wananchi wake,” amesema Rhoda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Mpanda, Halfan Zozi amesema, “Tuishi kama Watanzania, tupendane siasa iwe mchezo wa kukutana kwenye chaguzi anayekubalika afanye yake, anayekubalika kwa wananchi tumpe ushirikiano ili awafanyie kazi kwasababu wanamuamini.”

Winfrida Kusongwa, Mke wa Diwani Oscar aliishukru mahakama kutenda haki huku akibainisha changamoto zilizomkabili wakati mme wake alipokuwa gerezani.

“Nina watoto wane kati yao watatu wanasoma, nilikosa mahitaji ya kujikimu, nikawa nabangaiza kuuza pombe kutafuta kipato cha kulisha familia,Mungu ni mwema ameachiwa huru,” amesema Winfrida.