Aliyeongoza kumi bora Darasa la Saba 2020 afunguka

Aliyeongoza kumi bora Darasa la Saba afunguka

Muktasari:

“Nilimuahidi mama yangu kuwa nitakuwa Tanzania One kwa kuwa nilijua ninaweza kutokana na malengo yangu, walimu na maombi kwa Mungu.

Serengeti. “Likizo ya Corona niliitumia vizuri kusoma, maana matokeo ya mwaka jana ambayo Grace Imori alikuwa malkia wa nguvu yalinitia moyo ikizingatiwa kuwa alikuwa rafiki yangu,” ni maneno ya Herieth Josephat.

Herieth ambaye ni mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa katika Mtihani wa Taifa wa kuhitimu Darasa la Saba uliofanyika Oktoba Mwaka huu, anaendeleza rekodi ya Shule ya Msingi Graiyaki iliyoko wilayani Serengeti kwa kuwa mwaka 2019, mwanafunzi aliyeongoza ambaye alikuwa ni wa kike pia, alitoka shuleni hapo.

Amesema hakupoteza vipindi vyote vilivyopangwa na walimu, na wazazi wake walimwelewa nia yake wakampa nafasi ya kusoma.

“Nilimuahidi mama yangu kuwa nitakuwa Tanzania One kwa kuwa nilijua ninaweza kutokana na malengo yangu, walimu na maombi kwa Mungu. Aliyeongoza mwaka jana alikuwa rafiki yangu, nilimuahidi nami nafuata nyayo zake leo yametimia,” amesema Herieth alipozungumza leo Jumamosi Novemba 21, 2020 baada ya matokeo kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) nchini Tanzania.

Amesema kutokana na mikakati ya shule ya kuwa na mazoezi ya mara kwa mara kwa watahiniwa wote darasani,  alitegemea kufanya vizuri kwa kuwa wasichana na wavulana walikuwa na ushindani mkubwa.

Pili Wambura, mama yake mzazi amesema ushindi wa mtoto wake waliutegemea ingawa hawakujua kama angeongoza kitaifa.

“Pamoja na hali ngumu ya maisha, lakini tulijitahidi likizo ya corona kumlipia kwenye inteneti kusoma, leo matokeo yanaonekana,” ameiambia Mwananchi Digital mama huyo.

Mkurugenzi wa Shule za Graiyaki na Twibhoki, Grace Godfrey amesema siri ya mafanikio yao kwanza ni maombi kwa Mungu, walimu kujituma na wanafunzi kutambua kilichowapeleka shuleni hapo.

“Tumeingiza wasichana 7 na wavulana 3 wanafunzi bora kitaifa kwetu hii haikuja kwa bahati mbaya ni kutokana na uwajibikaji wa kila mmoja na wazazi kutimiza wajibu wao,” amesema.