Aliyepitishwa kuwania umakamu mwenyekiti halmashauri ya Songwe akataliwa

Wednesday November 25 2020
New Content Item (1)
By Stephano Simbeye

Songwe. Madiwani wateule wa CCM Wilaya ya Songwe wamempigia kura ya hapana diwani wa Mkwajuni, Shaibati Kapingu aliyependekezwa kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Songwe.

 Akizungumza leo Jumatano Novemba 25, 2020 msimamizi wa uchaguzi, Gerald Mwadalu amesema baada ya kuhesabu kura Kapingu alipata kura za ndiyo 11 huku za hapana zikiwa 14.

“Kutokana na kukataliwa nafasi ya makamu mwenyekiti itaendelea kuwa wazi,” amesema.

Mwadalu alimtangaza diwani mteule wa Mbangala,  Abrahamu Simbila kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo baada ya kupata kura 20 na kumshinda mpinzani wake  Michael Siwinga aliyepata kura 5.

Katika Halmashauri ya Mbozi msimamizi wa uchaguzi, Mery Mwasengo amtangaza George Msyani ambaye ni diwani mteule wa Nanyala kuibuka mshindi kwa kujipatia kura 25 dhidi ya kura 16 za mpinzani wake Maarifa Mwashitete.

Katika halmashauri ya  Ileje  msimamizi wa uchaguzi, Hebroni Kibona alimtangaza diwani mteule wa Luswisi,  Ubatizo Songa kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo baada ya kupata kura 14 dhidi ya kura saba za mpinzani wake, Gwalusakako Kapesa

Advertisement


Advertisement