Aliyetoroka nchini kwenda kuishi Dubai apandishwa kizimbani

Mshtakiwa Hasnei Mawji( wapili kutoka kulia) akiwa na ndugu zake katika Mahakaka ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya wizi wa Sh181 milioni.

Muktasari:

  •  Baada ya kutoroka nchini na kwenda kuishi Dubai miaka minne, Hasnei Shukat Mawji (39) maarufu Hasnei Shaukatali, amekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka mawili likiwemo la wizi wa Sh 181milioni ya kampuni ya Sanitary Appliance.


Dar es Salaam. Baada ya kutoroka nchini na kwenda kuishi Dubai miaka minne, Hasnei Shukat Mawji (39) maarufu Hasnei Shaukatali, amekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka mawili likiwemo la wizi wa Sh 181milioni ya kampuni ya Sanitary Appliance.

Mawji, ambaye ni meneja wa kampuni hiyo, amesomewa mashataka yake leo Jumatatu Juni 27, 2022 na wakili wa Serikali, Caroline Materu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rita Tarimo.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kutoroka nchini muda mfupi baada ya kuwekewa dhamana katika ya kesi ya jinai namba 373 ya mwaka 2018 yenye mashtaka ya wizi iliyokuwa inamkabili yeye na wenzake wawili katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikamatwa wiki mbili zilizopita katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ulipo Jijini Dar es Salaam (JNIA) wakati akijiandaa kwenda Pakistani kusalimia familia yake.


Baada ya kukamatwa mshtakiwa huyo ameunganishwa na wenzake wawili wanaokabiliwa na kesi ya wizi katika Mahakama ya Kisutu.

Akimsomea mashtaka yake, wakili Materu amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa kesi ya Jinai namba 18/2020.

Katika shtaka la kwanza, Mawji na wenzake Festo Kasasa(55) ambaye ni dereva na mkazi Majohe pamoja  na Hassan Amirali(49), ambaye ni Msimamzi wa kampuni hiyo, wanadaiwa Januari 11, 2018 katika jiji la Dar es Salaam walikula njama za kutenda kosa.

Shtaka la pili, washtakiwa kwa pamoja waliiba vitu mbalimbali ikiwemo nyaya ambazo hazishiki kutu zenye thamani ya Sh 181,985,000 mali ya kampuni ya Sanitary Appliance and Hardware Limited.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake alikana kutenda kosa hilo.

Wakili Materu amedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali mshtakiwa.

Pia Materu ameiomba mahakama hiyo isimpe mshtakiwa huyo dhamana kutokana na kuruka dhamana katika kesi wizi ilivyokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.