Anaswa na kete 2,400 za heroin Zanzibar

Muktasari:

  • Mkazi wa Nungwi kisiwani Zanzibar, Athumani Akida Juma (32) amekamatwa na pakiti 20 zenye kete 2,401 zinazodaiwa ni dawa za kulevya aina ya heroin.

Unguja. Mkazi wa Nungwi kisiwani Zanzibar, Athumani Akida Juma (32) amekamatwa na pakiti 20 zenye kete 2,401 zinazodaiwa ni dawa za kulevya aina ya heroin.

 Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar, Kanali Buruhani Zuberi Nassoro wakati akizumgumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Septemba 22, 2022 mjini Unguja.

Amesema kijana huyo amekamatwa katika operesheni na doria za ukamataji wahalifu wanojihusisha kuuza na kusambaza dawa ya kulevya nchini.

“Pia katika operesheni hiyo tumekamata mzigo kisiwani Pemba uliotelekezwa ukiwa na kete 4,000 za bangi huku upelelezi ukiendelea kwa kutafuta mwenye mzigo huo,” amesema

Kanali Nassoro amesema kuwa wataendelea kushirikiana na mamlaka zote zinazohusika kudhibiti vitendo hivyo.