Anayedaiwa kukutwa na nyeti, mafuvu ya binadamu afutiwa kesi

Muktasari:

  • Kijana Nkonja hadi anafutiwa kesi yake na kuachiwa huru, amekaa rumande kwa muda wa miaka saba tangu 2017.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi na kumwachia huru mshtakiwa Salum Nkonja (23) maarufu kama Emmanuel Nkonja, aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka 11 yakiwemo ya  kukutwa  na vipande viwili vya mafuvu ya vichwa vya binadamu pamoja na sehemu za siri tano za mwanamke (Uke), baada ya kesi hiyo kuahirishwa zaidi ya mara tano bila kuendelea na ushahidi.

 Uamuzi huo umetolewa leo, April 17, 2022 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Ramadhani Rugemalira wakati kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 32/2022 ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Mbali na kumfutia mashtaka na kumwachia huru, mshtakiwa hiyo, Mahakama hiyo imeamuru mshtakiwa asikamatwe mpaka upande wa mashtaka watakapowasilisha vielelezo mahakamani hapo.

"Mshtakiwa huyu alifikishwa mahakamani hapa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na kufunguliwa kesi ya mauaji namba 21/2017 na Novemba 19, 2017 Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliifuta kesi hii na kumfungulia kesi ya uhujumu uchumi namba 88/2020 ambayo nayo ilifutwa na Mahakama hii Juni 7, 2022 na mshtakiwa kurudishwa Kituo cha Polisi ambapo alikaa huko kwa siku 14 na Juni 21, 2022 aliletwa mahakamani na kufunguliwa kesi nyingine ya uhujumu uchumi namba 32/2022" Amesema hakimu Rugemarila.

"Hivyo tangu Jun 22, 2022 kesi  imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kuendelea na ushahidi kutokukana na wakati mwingine mashahidi wanakuja mahakamani hapa lakini vielelezo vinakuwa havipo, hata leo shahidi wa upande wa mashtaka Koplo Seleman yupo lakini hawawezi kuendelea na ushahidi kwa sababu hawana vielelezo" amesema Hakimu Rugemira.

Amesema hali hiyo haiwezei kuvumuliwa na Mahakama hiyo kwa sababu mshtakiwa pia ana haki, hivyo aliamua kuifuta kesi hiyo ambayo ilishaanza kusikilizwa ushahidi.

Kabla ya kufutwa kwa kesi hiyo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili kuendelea na ushahidi na tayari shahidi wa pili katika kesi hiyo Koplo Selemani yupo Mahakamani lakini vielelezo vya shauri hilo havijaletwa, hivyo wanaomba kuahirishwa kwa shauri hilo.

Kutokana na hali hiyo, wakili wa Utetezi Mohamed Majaliwa alidai kuwa kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara hivyo anaomba kesi hiyo iendelee kusikilizwa.

Hakimu Rugemalira baada ya kusikiliza maeneo ya pande zote, alipitia jalada la kesi hiyo kwa kusoma kila ukurasa huku akitaja tarehe tofauti tofauti za kesi hiyo kuahirishwa bila kuendelea na kujirisha kuwa kesi hiyo imeahirishwa mara nyingi na kisha kuandika uamuzi.

Itakumbukwa kuwa Machi 20, 2023 shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka Leticia Waitara(40) ambaye ni Mtaalamu wa Vinasaba( DNA) kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, alitoa ushahidi wake dhidi ya mashtaka hayo.

Katika ushahidi wake, Waitara alidai Novemba 3, 2017 akiwa Kitengo cha Baiolojia  vinasaba( DNA), alipokea kifurushi kilichokuwa kimewekwa kwenye bahasha ya khaki ambapo ndani yake kulikuwa na vielelezo vitatu ambavyo ni sehemu za siri tano za mwanamke( uke) chuchu mbili binadamu na vipande viwili vya mafuvu ya binadamu

Pia kifurushi hicho lilikuwa kimeambatana na barua kutoka forensic Bureau, barua kutoka kwa Mkuu Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam pamoja na Form 180.

"Barua hizo zilikuwa zinataka nifanye uchunguzi kujua kama viungo hivyo ni vya binadamu au la" alidai Waitara.

Waitara alidai baada ya kupokea vielelezo hivyo ambavyo vilikiwa ni viungo vikavu na kuviwekea alama za utambuzi ambazo ni A, B na C.

"Vipande viwili vya fuvu nilivipa alama A, sehemu tano za siri za mwanamke nilivipa alama B na chuchu mbili za binadamu nilizipa alama C" alidai Waiatana na kuongeza

"Baada ya kuviwekea alama vielelezo hivyo, nilianza kuvifanyia uchunguzi kwa kutumia teknolojia ya Vinasaba vya binadamu" alidai Waitara ambaye aliajiriwa na Mamlaka hiyo ya Mkemia wa Serikali mwaka 2008.

Alidai Novemba 8, 2017 alimaliza kufanyia uchunguzi wa kielelezo hicho na kisha kuandika ripoti ya uchunguzi.

Hata hivyo aliulizwa na wakili wa Serikali Mosei Kaima, uchunguzi wake aliofanya ulibaini kitu gani? Shahidi huyo alijibu kuwa uchunguzi ulibaini kuwa viungo hivyo ni masalia ya kweli ya binadamu.

"Uchunguzi wa kitaalamu niliyoufanya ulinionyesha kuwa viungo hivyo vyote ni masalia halisi ya viungo vya binadamu mwenye jinsia ya kike" alidai Waitara ambaye ana shahada ya pili ya Biotechnology aliyoipata mwaka 2016 kutoka chuo cha LUND kilichopo nchini Sweeden.

Shahidi aliomba mahakama ipokee ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na viungo hivyo vya binadamu kuwa vielelezo vya Mahakama, ombi ambalo lilikubaliwa.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa yake kati ya Oktoba 30 na Novemba 30, 2017 katika eneo la Ubungo, Jijini Dar es salaam.

Mbali na kukutwa na viungo vya binadamu, Nkonja anadaiwa kukutwa na  pembe moja ya Nyati ; uume wa mbwa; uume wa Nyumbu; mikia mitano ya Ngiri; Yai moja la Mbun; uume tatu za fisi na kichwa kimoja cha nyoka aina ya Cobra, vyote mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.