Anayedaiwa kutengeneza radi auawa na wananchi

kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Sylvester Ibrahimu

Muktasari:

  • Baraka Said (30) mkazi wa kijiji cha Mtisi halmashauri ya Nsimbo ameuawa na wananchi  baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kwenye paji  la uso na kupigwa na kitu kizito kisogoni  akituhumiwa kujihusisha na ushirikina wa kutengeneza radi.

Katavi. Baraka Said (30) mkazi wa kijiji cha Mtisi halmashauri ya Nsimbo ameuawa na wananchi  baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kwenye paji  la uso na kupigwa na kitu kizito kisogoni  akituhumiwa kujihusisha na ushirikina wa kutengeneza radi.

Akizungumza na wanahabari leo Januari 29, 2022 kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Sylvester Ibrahimu amesema tukio hilo limetokea Januari 24, 2022 saa 12 jioni kijijini hapo.

Amesema wananchi hao walimtuhumu marehemu kutengeneza radi iliyompiga Anjelina Revocatus (16) mkazi wa kijiji hicho na kusababisha kifo chake wakati anatibiwa hospitali ya rufaa Mkoa wa Katavi.

"Watuhumiwa nane wamekamatwa,John Mayonjuwa, Mashaka Mathias, Sele Richard, Revocatus Reymond, Julias Dalali, Hawa Rashid, Agnes Rashid na Tausi Abdu. Upelekezi ukikamilika watafikishwa mahakamani," amesema Ibrahimu.

Katika tukio jingine Ibrahimu amesema nyumba 10 zilizojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi kijiji cha Igongwe zimechomwa moto na kuteketeza mali zote zilizokuwa ndani.

Amesema  tukio hilo limefanywa na baadhi ya wananchi wa Stalike waliojichukulia sheria mkononi wakigombania mashamba kati yao na  kijiji cha Igongwe lililopelekea  kifo cha Klisent Mwananjela (40) mkazi wa kijiji cha Stalike.

" Katika tukio hilo la mauaji chanzo chake ni kuchomwa nyumba kwa moto hali iliyosababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia wahalifu na kupelekea kifo cha Klisent,"

Aidha amesema watu saba wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo la mauaji akiwamo Mtanda Yegela (19) mkazi wa Itenka A, Maico Kihongwe (48) mwenyekiti wa kijiji cha Muungano na Lucas Shabai (22) mkazi wa kijiji cha Mnyamasi.

Wengine ni James Charles (23) mkazi wa kijiji cha Itenka, Salula Tano (27) mkazi wa kijiji cha Itenka, Frederick Edward (26) mfanyabiashara wa Ubilimbi Kahama na Samwel Maico (44) mkazi  wa Itenka.

" Watuhumiwa wote  watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika kujibu tuhuma zinazowakabili na juhudi za kuwasaka wengine waliosababisha mauaji zinaendelea," amesema.

Sanjari na hayo watuhumiwa nane wamekamatwa kuhusika na tukio la kuchoma moto nyumba 10  mali ya Sayi Wema mkazi wa kijiji cha Igongwe.

"Walitekeleza nguo, mazao ya mahindi na mpunga thamani yake haijapatikana,"

"Tumewakamata Daud Gembe (54) mkazi wa kijiji cha Stalike,Abas John (30)mkazi wa kijiji cha Stalike,Genius Sindani (65)mkazi wa Stalike, Julia's Nicolaus (38) mkazi wa kijiji cha Stalike na Japhari Razaro (48) mkazi wa Vikonge."

"Godfrey Basili(44)mkazi wa Stalike,Joseph Leopard (33) mkazi wa Stalike na Klisent Mwananjela (40) mkazi wa Stalike,watuhumiwa wote wamefikishwa mahakama ya mkoa kujibu mashtaka hao,"

Kufuatia uwepo wa matukio hayo ametoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kitendo kinachosababisha kujeruhi na mauaji.