Anuani za makazi kukamilika miezi mitano

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akiteta jambo na  Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye  baada ya kufungua mafunzo elekezi ya utekelezaji mfumo wa anuani za makazi. Picha na Julieth Ngarabali.

Muktasari:

Nape asema sasa Mradi wa mfumo wa anuani za makazi utafanyika kwa miezi mitano tuu badala ya miaka mitano iliyokua imepangwa.

Pwani. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali imeamua kutekeleza mradi wa  kuweka mfumo wa anuani za makazi kwa muda wa miezi mitano badala ya miaka mitano ilivyokuwa imepangwa kwa sababu ni muhimu katika kusaidia sensa ya watu na makazi kufanyika kwa usahihi.

 Nape amesema hayo leo Januari 18, 2022 mjini Kibaha akifungua semina ya utekelezaji mfumo huo katika mkoa wa Pwani na kusema lengo lake ni kuhakikisha kila mwananchi wa nchi hii anapatikana katika anuani fulani .

Waziri huyo amebainisha kuwa anuani hizo za makazi zimekusudiwa kuwekwa kwenye maeneo ambayo wananchi wanaishi, wanafanya biashara na shughuli zao mbalimbali.

"Sasa huu ni mradi mkubwa lengo lake ni kufanyika nchi nzima na ulikuwa ufanyike kwa miaka mitano lakini tumeamua kuufanya kwa muda mfupi hadi kufikia Mei 22 mwaka huu mradi uwe umekamilika kwa sababu ni mradi muhimu katika kusaidia sensa ya watu na makazi kufanyika kwa usahihi"amesema Nape

 Amewataka viongozi wa mkoa wa Pwani kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo.

‘’Hapa hautuna kitu kingine zaidi ya utekelezaji wa mradi huu, iwe mvua, iwe jua lazima jambo hili litekelezwe, Pwani mko nyuma sana mna kata 3 ambazo zimetekeleza jambo hili na nguzo 439 zimewekwa lakini  bado kata 139, mahitaji yenu ni nguzo 75,392 na vibao 912,640 kwa hiyo utekelezaji wenu umefikia asilimia 1 bado asilimia 99”, amesema Nape.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema uwekeji wa anuani za makazi na postikodi utarahisisha utambuzi maeneo ya shughuli mbalimbali mkoani humo yakiwamo maeneo ya viwanda.

"Huu mradi lazima utekelezaji wake tuuchangamkie ipasavyo, maana anuani za makazi na postikodi ni mfumo mzuri ambao utatuonesha maeneo yetu mbalimbali kama mnavyofahamu Pwani ina viwanda vingi sana kwa hiyo itawarahisishia wananchi na zitarahisisha usafirishaji wa bidhaa katika maeneo yetu”, amesema Kunenge