Anusurika kifo akijaribu kujinyonga, kisa ugomvi na mama yake

Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Mpomvu mjini Geita wakimtazama mwanamke anayedaiwa kutaka kujinyonga baada ya kuchoshwa na manyanyaso kutoka kwa mama yake mzazi.

Muktasari:

 Regina Jumanne (28) amesema alitaka kujiua baada ya kuchoshwa na manyanayaso kutoka kwa mama yake mzazi ambaye humtukana mara kwa mara akidai yeye sio mtoto wake.

Geita. Mkazi wa Mtaa wa Mpomvu uliopo katika kata ya Mtakuja mjini Geita, Regina Jumanne (28) amenusurika kifo baada ya kuokolewa na wasamaria wema wakati akiwa amepanda juu ya mwembe kwa lengo la kujinyonga.

Mwanamke huyo akizungumza kwenye ofisi ya uongozi wa mtaa huo, amesema ametaka kujiua baada ya kuchoshwa na manyanayaso kutoka kwa mama yake mzazi, ambaye humtukana mara kwa mara akidai yeye sio mtoto wake.

“Sina maelewano na mama yangu mzazi, vikwazo ni vingi, mama ananikataa na kunifukuza nyumbani akidai mimi sio mwanaye, mimi sina baba.Nimetoka kwenye ndoa nikiwa mjamzito, nimejifungua nalea mwanangu lakini kila siku vikwazo. Nawaza wazazi wangu wako wapi, yeye anampendelea mmoja tu, akisikia neno mtaani anaanza kuja na kunitukana hata kama ni la uongo,” amesema Regina.

Andera Machbula ambaye ni balozi wa eneo hilo, amesema mama huyo akiwa juu ya mti alifunga kitenge juu ya tawi, wapita njia wakamuona na kupiga yowe lililosaidia watu kumuokoa, na alipoulizwa alidai amechoshwa na manyanyaso kutoka kwa mama yake.

“Alipokuwa anaulizwa sababu za kujinyonga alidai shida kubwa ni mama yake kudai anatembea na hawara yake, jambo ambalo sio kweli na tulichofanya ni kuwakutanisha na kila mmoja kueleza changamoto zake na tulipowafikisha kwenye ofisi ya mtaa tuliwasuluhisha na kuwataka waelewane lisijirudie tena.

“Tumemtaka mama ajue familia yake na asibague mtoto, kama kuna baya ashirikishe watu au hata viongozi ili tutafute ufumbuzi badala ya kukaa na tatizo na kuchukua uamuzi wa kujiua, uamuzi ambao ni mbaya,” amesema Machbula.

Kwa upande wake, mama mzazi wa Regina, Chausiku John amekana madai ya mwanawe na kusema  aliamua kujichukulia uamuzi ya kujinyonga bila kumshirikisha mtu, lakini ameshamsamehe na ana imani wataendelea kuishi kwa amani.

“Tatizo ni kero za nyumbani tu, tulikuwa wote ndani akatoka tukamfuatilia ndiyo tukamkuta kwenye mwembe tukapiga yowe, watu wakaja wakamtoa, akaletwa ofisini. Nimewasamehe lakini nimewaambia waache maneno ya kunisema vibaya,” amesema Chausiku.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mpomvu, Mathias Mwetusela amekiri kuwapokea mama na mwanae aliyetaka kujinyonga na kusema katika mahojiano yao amebaini chanzo ni mgogoro wa kifamilia.

Amesema kama viongozi wamekaa na familia hiyo na kuwaasa kuwa na upendo na umoja na kuwashauri pale wanapokuwa na changamoto ni vema wakaomba ushauri kwa mtu awasikilize badala ya kuamua kujichukulia uamuzi wa kujitoa uhai ambayo pia ni kosa kisheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo alipoulizwa kuhusu tukio hilo amesema hana taarifa na kuahidi kulifuatilia na kusema inapotokea tukio halijaondoa uhai jamii hupenda kulimaliza wenyewe.

Amesema kitendo cha mtu kutaka kujiua ni kosa la jinai na jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine na kuwataka viongozi wa mitaa kutomaliza matukio kama hayo kimyakimya kwa kuwa yataendelea kutokea endapo hatua stahiki hazitachukuliwa.

Wakati huohuo, mwanaume mmoja mkazi wa Bwanga wilayani Chato anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumjeruhi vibaya aliyekuwa mke wake kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kwenye ziwa lake la kushoto kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda Jongo amesema mwanaume huyo alipata taarifa za kuwa aliyekuwa mke wake aliyetambulika kwa jina la Veronica Machage (24) ameanza mahusiano na mtu mwingine ndipo alipokwenda kwenye eneo analofanya biashara ya kuuza uji na matunda na kumchoma kisu kwenye ziwa la kushoto kwa lengo la kumuua.

“Kwa bahati nzuri mwanamke huyu hakufa na anaendelea na matibabu kwenye kituo cha afya Bwanga. Alipomchoma kisu alikimbia lakini tumemsaka na jana tumemkamata tunaendelea na taratibu za kumfikisha Mahakamani,” amesema Kamanda Jongo.