Apandishwa kizimbani kwa madai ya kumpa ujauzito mwanafunzi

Muktasari:

  • Mkazi huyo wa Chamazi amefikishwa mahakama ya Temeke na mashtaka mawili likiwemo la kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari Magonza mwenye umri wa miaka 16.

Dar es Salaam. Mkazi wa Chamazi jijini hapa, Raymond Dastan 24 amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Temeke akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari Magonza mwenye umri wa miaka 16.

Akisoma hati ya mashitaka leo Agosti 30 katika mahakama hiyo, Wakili wa Serikali, Eric Shija amedai kati ya Juni 18 na Julai 24, 2021 maeneo ya Chamazi wilaya ya Temeke mshtakiwa huyo alimbaka na kumpa mimba mwanafunzi huyo.

Shija amedai upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo ameiomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi, Anna Mpesa amesema dhamana ipo wazi hivyo mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaotakiwa kuwa na vitambulisho vya taifa na kila mmoja atasaini bondi ya Sh2 milioni.

Mpesa alihairisha shauri hilo hadi Sepetemba 13, 2021 wanakapokuja kwa ajili ya kumsimea mshtakiwa maelezo ya awali.