Arizona jimbo la 15 Marekani kuruhusu bangi

Dar es Salaam. Katika siku ya kwanza baada ya Jimbo la Arizona nchini Marekani kuruhusu uuzaji wa bangi, zaidi ya watu 50 walinyeshewa na mvua wakiwa kwenye foleni ya kununua bidhaa hiyo katika moja ya maeneo yaliyoruhusiwa juzi.

Baadhi yao walikuwa kwenye foleni kwa zaidi ya saa moja au zaidi, lakini walikuwa na furaha kwa kuwa ilikuwa mara yao ya kwanza kuuziwa bangi katika zahanati. Wagonjwa wanaohitaji bangi kwa ajili ya dawa pia walikuwapo, lakini baadhi yao walikasirika kwa kusubiri zaidi ya kawaida.

Jimbo la Arizona limeidhinisha uuzaji wa bangi kwa matumizi bangi ya starehe na kuweka rekodi ya kuwa jimbo la 15 nchini humo kupitisha sheria inayoruhusu matumizi ya bangi.

Nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania zimepiga marufuku matumizi na biashara ya bangi kwa sababu mmea huo uko kwenye kundi la dawa za kulevya na unasadikiwa kusababisha madhara kwa watumiaji wake.

Hata hivyo, jitihada hizo za mataifa bado hazijafanikiwa kwa sababu mmea huo haramu bado unazalishwa kwa wingi, biashara zinafanyika na baadhi ya watu wanakamatwa aidha kwa kulima au kuuza bangi.

Majimbo 15 kati ya 50 ya Marekani, yameruhusu matumizi ya bangi, pia, mataifa mengine kama vile Canada, Jamaica, Argentina, Mexico, Colombia, Ecuador, Peru na Uruguay nayo yameruhusu matumizi ya bangi kwa starehe.

Baadhi ya mataifa hayo yameruhusu kiasi matumizi ya bangi kwa kati ya gramu tano hadi 20 huku wakulima wakitakiwa kusajiliwa rasmi kama wazalishaji wa mmea huo.

Ijumaa iliyopita, jimbo la Arizona lilipitisha rasmi sheria ya kuruhusu bangi kuuzwa kwa matumizi ya starehe.

Idara ya Huduma ya Afya katika jimbo hilo ilitangaza kuwa tayari imeidhinisha leseni 86 katika kaunti tisa kati ya 15 chini ya vifungu vya sheria iliyohalalisha bangi kama ilivyopitishwa na wapigakura Novemba mwaka jana.