Asilimia 97 ya wagonjwa wa haemophilia hawajijui

Muktasari:

  • Haemophilia ni ugonjwa unaotokana ukosefu wa chembechembe zinazosaidia damu kuganda. Mtu anazaliwa akiwa hana chembechembe zinazogandisha damu hivyo anapopata jeraha anapoteza damu nyingi hali inayoweza kumletea hatari mwilini.

Dar es Salaam. Licha ya Tanzania kukadiriwa kuwa na wagonjwa wa Haemophilia 6000, wanaotambulika hadi sasa ni wagonjwa 167 sawa na asilimia 2.78 pekee wengi wao wakiwa wa maeneo ya mijini.


Hali hiyo inatokana na watu wengi kutofahamu kuwa wana ugonjwa huo na hata wataalam wa afya kushindwa kugundua dalili zake kwa haraka.


Hayo yalielezwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya damu, Stella Rwezaura wakati akitoa mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa wa haemophilia kwa wataalam wa afya wa jiji la Dar ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupambana na ugonjwa huo.


Dk Stella alisema ugonjwa huuo wa kurithi ni miongoni mwa magonjwa ambayo hajazoeleka kwenye jamii hivyo kuwawia vigumu wataalam wa afya ambao hawajabobea kuubaini na kumuanzishia mgonjwa matibabu.


Kutokana na hilo wagonjwa wengi hufika hospitali kwa kuchelewa hali inayowasababishia wengine kupata ulemavu na hata kupoteza maisha.

Alisema kukabiliana na shirika la Novo Nordisk Haemophilia Foundation kwa kushirikiana na  Chama cha Madaktari wa magonjwa ya damu wanatekeleza mradi wa kuongeza kasi ya kutoa huduma kwa magonjwa hayo.


Sanjari na hilo, mradi huo unalenga pia kufanya tafiti ili kupata takwimu sahihi za watu wenye ugonjwa huo na wanakopatikana ili waweze kufuatiliwa na kuhakikisha wanapata matibabu stahiki.


 “Tunataka katika hospitali zote za rufaa kuwe na kliniki ya magonjwa haya ambako kutakuwa na madaktari waliobobea, ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kuja Muhimbili,” amesema Dk Stella.


Kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume alisema ni muhimu kwa wazazi kuwawahisha watoto wao hospitali pale wanapoona mwenende usio wa kawaida wa afya zao.


Alisema, “Changamoto ni kwamba wanauumwa wengi hawajitambui kwa mfano Dar es Salaam tunakadiria kuwa na wagonjwa 600 lakini waliosajiliwa na kutambuliwa hadi sasa ni 60 pekee, unaweza kujiuliza hao wengine wako wapi na wana hali gani,” amesema Mfaume.

Abdulsadik Mgazambina ambaye ni mmoja wa wagonjwa wa Haemophilia alieleza kuwa amekuwa na maisha magumu kutokana na kuishi na ugonjwa huo unamsababishia kushindwa kufanya baadhi ya kazi.


“Sitakiwi kupata jeraha la aina yoyote, hivyo kuna kazi nashindwa kufanya, mwili wangu umekuwa na maumivu siku zote na maisha yangu yanategemea dawa, sina la kufanya kwa sababu nimezaliwa hivi,” alisema Mgazambina.