Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Asimulia alivyosota gerezani miaka 30 akisubiri kunyongwa

Faris Lyimo

Muktasari:

  • Maisha ni safari ndefu, hivyo ndivyo unavyoweza kusema unapokutana na simulizi ya Faris Lyimo, mkazi wa Njoro Manispaa ya Moshi, aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya mfanyabiashara wa duka la vinywaji.

Moshi. Maisha ni safari ndefu, hivyo ndivyo unavyoweza kusema unapokutana na simulizi ya Faris Lyimo, mkazi wa Njoro Manispaa ya Moshi, aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya mfanyabiashara wa duka la vinywaji.

Lyimo, ambaye alikuwa mfanyabiashara wa mitumba katikati ya mji wa Moshi, alikutwa na madhila hayo mwaka 1991, baada ya kutokea tukio la mauaji ya mfanyabiashara katika moja ya baa iliyokuwa eneo la Majengo kwa Mtei.

Kwa miaka takribani 30, Lyimo amekuwa gerezani akilala usingizi wa maruweruwe akisubiri kutekelezwa kwa adhabu yake ya kunyongwa, hadi alipoachiwa kwa msamaha wa Rais Samia Suluhu Hassan siku ya Uhuru Desemba 2021.

Miaka sita alisota gerezani akisubiri hatima ya kesi yake kuanzia tangu akamatwe mwaka 1991 na kesi kusikilizwa na kutolewa hukumu mwaka 1997 na kukaa gerezani akisubiri kunyongwa.

Muda wote baada ya kukamatwa, kushtakiwa na hatimaye kuhukumiwa adhabu ya kifo, mzee huyo ambaye sasa ana miaka 60 baada ya kukamatwa akiwa na miaka 27, amekuwa akikana kuhusika na mauaji na hadi sasa anayakanusha.

Badala yake, anasema kilichomponza ni urafiki wa karibu na rafiki yake waliyehukumiwa naye adhabu hiyo, ambaye mashahidi wa kesi hiyo walimuunganisha naye, licha ya kwamba yeye hakuwepo eneo la mauaji.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Lyimo anasema miaka 30 aliyokaa gerezani huku akihamishwa magereza tofauti, imekuwa michungu kwake, kwa kuwa hakutenda kosa hilo wala kulishuhudia kwa namna yoyote.

Mzee Lyimo na mwenzake Jullius Philipo, walihukumiwa adhabu ya kifo mwaka 1997 na Jaji Nathaniel Mushi, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara mmoja mkazi wa Majengo Kwamtey, Hasara Athman.


Akisimulia tukio lilivyokuwa

Lyimo anaeleza kuwa, mwaka 1980 alipomaliza elimu ya msingi, alijihusisha na biashara ya kuuza mitumba maeneo ya Stendi mjini Moshi, baadaye alikutana na rafiki yake waliyesoma wote na kuanza biashara pamoja.

“Baada ya kukutana aliniomba tufanye biashara pamoja, mimi nilimkaribisha na biashara iliendelea na tulikuwa tunapata fedha, basi tukawa tumepanga sehemu za kwenda kunywa baada ya kumaliza kazi zetu,” anasema mzee Lyimo.

“Tulikuwa tunaenda sehemu ambayo marehemu aliuawa na wakati huo watu walituzoea sana kwenye ile baa na tulikuwa tukifika pamoja na rafiki yangu,” anasema mzee Lyimo, akimaanisha baa iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu.

“Lakini kuna wakati mwingine rafiki yangu alikuwa ananiacha mimi kazini anakwenda peke yake, sasa ikiwa anafika pale na kunywa pombe na wakati mwingine alikuwa anakopa halipi akawa anadaiwa fedha.”

Akinukuu maneno aliyoelezwa baada ya tukio la mauaji na aliyoambiwa na rafiki yake waliyehukumiwa pamoja adhabu ya kifo, anasema siku ya tukio, marehemu alishanoa panga ili kumwadhibu rafiki yake kwa kutolipa deni.

“Marehemu akawa amewaambia watu kwamba mtu fulani namdai akija hapa leo kama hatanipa fedha yangu namuua, sasa wakati anasema hivyo alikuwa ananoa panga lake na watu wakiwa wanamuona,” anasimulia mzee Lyimo.

“Baada ya kuongea na watu, huyu rafiki yangu alikuwa hajapata hizo habari, yeye akawa ametoka hapa kazini akawa ameenda pale. Hapo ndio niliambiwa marehemu alitoa panga na kumtaka amlipe fedha za pombe anazomdai.

“Yule bwana ikabidi atoe pochi yake na kuitupa chini huku akimwambia kama ni fedha zako chukua bwana,” anasimuliza mzee Lyimo akinukuu kile alichoelezwa na rafiki yake huyo wakiwa gerezani.

“Sasa huyu bwana alibahatika kutoka nje na kuchukua mawe akamrudia yule mwenye baa aliyemkata na panga mkononi akamwambia kwa sababu umeshanijeruhi bora tuuane.

“Yule bwana kwa kuwa alikuwa na panga bado alitoka na panga lake mbio huku huyu rafiki yangu akimrushia mawe; jiwe lilimpata kichwani na kudondoka chini. Alipodondoka aliokota lile panga akamkata shingo akafa pale pale.

“Muda huo giza lilikuwa tayari limeshaingia, akapata mwanya wa kutoroka akaenda kujificha mbali, watu waliofika eneo lile wakawa wanajiuliza huyu aliyetenda hiki kitendo ni nani? Wakamtaja huyu rafiki yangu.

“Kukawa kuna watu wako pale wakasema kuna kijana anakuja naye lakini hatujui sehemu anayoishi, pale pale wakasema waje wanikamate mimi kwa sababu nilikuwa najulikana nakaa wapi basi wakaja kunitafuta.

“Walinitafuta na kesho yake nikiwa kwenye biashara yangu nikakamatwa na polisi na kuingizwa kwenye tukio ambalo sikuhusika na silijui, nikafikishwa Kituo cha Polisi cha Majengo na ilikuwa mwaka 1991.”

Lyimo anasema baada ya kufikishwa polisi aliulizwa maswali huku akiambiwa hataachiliwa hadi rafiki yake atakapojisalimisha.


Alivyokutana na rafiki yake gerezani

Mzee Lyimo anasema ilichukua kama miezi mitano au sita tangu akamatwe na kushtakiwa kwa mauaji hayo ndipo alipokutana na rafiki yake huyo baada ya kukamatwa na kuletwa mahakamani kwa ajili ya kuunganishwa katika kosa hilo.

“Wakati ma-file (majalada) yanasomwa yule mwendesha mashtaka akasema kuna mshtakiwa mwingine hapa, wanataka kuniunganisha naye kwenye kesi ya kuua, ndipo nikaunganishwa naye tukarudishwa tena Gereza la Karanga.

“Mwaka 1997 mbele ya jaji mashahidi wakaanza kutoa ushahidi wao wakieleza namna huyu rafiki yangu alivyoua, na kwa kuwa walizoea kuniona naye na mimi nikaunganishwa.

“Baadaye nilitoa ushahidi wangu lakini sikupata wa kunitetea, nikaingizwa kwenye hatia ambayo sikuhusika. Mwaka huo huo 1997 nilihukumiwa mimi na rafiki yangu kunyongwa hadi kufa.”


Alipotoka gerezani

Lyimo ambaye aliacha mke na mtoto mmoja wakati anakamatwa, anaeleza kuwa, alipotoka gerezani hali aliyoikuta nyumbani ilikuwa ni ngumu kwa kuwa alikuta mke kaondoka na hata vitu vyake alivyoviacha nyumbani hakuvikuta.

“Nilimuacha mwanangu akiwa na miaka sita, na wakati narudi mwaka jana alikuwa na miaka 36, lakini sikumkuta mke wangu, nilikuta alishaondoka na ana watoto wengine wakubwa, mali zangu nazo nilikuta hazipo,” anasema Lyimo.

“Nilikuta nyumba imebomoka, hata mdogo wangu aliyenifuata nilikuta amefariki dunia. Maisha kwa sasa ni magumu, ningeomba Serikali inisaidie.”

Mzee Lyimo anasema Marangu anakoishi kuna shamba, lakini anashindwa hata kulima kutokana na kukosa kipato cha kumuwezesha kulima.

“Nikiwa gerezani nilikuwa nafanya kazi mbalimbali katika kiwanda na hata kulima, kwa hiyo japo kilikuwa ni kilimo cha adhabu, kimenifundisha kuwa muda mrefu katika kazi, hivyo kwa sasa napenda kufanya kazi sio kuzunguka bila kufanya kazi.”

Anasema jambo ambalo hatalisahau katika maisha yake ni mateso aliyopitia gerezani, wakati akidai haki yake, kitu kilichomuathiri kutojipenda.